Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
“Ni furaha kubwa kuungana nanyi katika utoaji wa Tuzo mbalimbali ambazo ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango na mafanikio yenu katika utoaji wa habari na taarifa za hali ya hewa kwa Jamii”.
Hayo yalisemwa na mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi wakati wa hafla ya utoaji tuzo ya mwanahabari bora wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2023, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Biashara (CBE), Dar es Salaam, Tarehe 30 Oktoba 2023.
Katika utoaji wa tuzo hizo, mshindi wa tuzo ya jumla alikuwa Bw. Mussa Kharid kutoka Kiss FM, mshindi wa upande wa magazeti alikuwa Bi. Pamela Chilongola kutoka gazeti la Mwananchi na mshindi wa upande wa mitandao ya kijamii alikuwa Noel Rukanuga kutoka Uhondo TV.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang’a aliwaeleza wanahabari kuwa Mamlaka itaendelea kuboresha na kupanua wigo wa Tuzo za Wanahabari Bora wa taarifa za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kadri inavyowezekana, na aliwaomba wanahabari watoe maoni na mapendekezo ya namna bora ya kupanua wigo wa utoaji Tuzo ili kuendelea kuchagiza mwamko na umahili katika kutoa elimu na kusambaza tarifa za hali ya hewa.
Hafla hiyo fupi ilifanyika wakati wa warsha ya wanahabari kuhusu utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka kuanzia mwezi Novemba 2023 hadi Aprili 2024.
0 Comments