TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema marehemu Dkt. Faustine Ndugulile alikua kiongozi mwenye nidhamu, rafiki wa kila mtu na kiongozi aliyeweza kutetea vema maslahi ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo alipofika nyumbani kwa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika Dkt. Faustine Ndugulile Kigamboni Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuifariji familia pamoja na waombolezaji wote.
Makamu wa Rais amewaombea faraja na moyo wa uvumilivu wote walioguswa na msiba huo. Amewashukuru wote walioshiriki katika kuifariji familia wakati huu wa kipindi kigumu kwao na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana katika nyakati mbalimbali zinazojitokeza katika jamii ikiwemo za majozi na furaha.
Aidha amesema inapaswa kuendelea kumshukuru Mungu kwa maisha ya Dkt. Ndugulile hapa duniani. Ameongeza kwamba ni vema kwa Watanzania kuendelea kuishi vizuri na ndugu na majirani.
Akiwa nyumbani hapo, Makamu wa Rais amesali pamoja na familia, ndugu, jamaa na marafiki kumuombea marehemu Dkt. Faustine Ndugulile.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
30 Novemba 2024
Kigamboni – Dar es Salaam.
0 Comments