Na mwandishi wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kuwa mitaala inayoandaliwa ihakikishe inazingatia mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya kiteknolojia.
Amesema hayo leo (Ijumaa, Novemba 22, 2024) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kongamano la tano la Maendeleo ya Biashara na Uchumi linalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hazina jijini Dodoma.
Amesema kuwa kuna umuhimu wa kutumia teknolojia katika kuboresha elimu ya biashara kwa kutumia jukwaa la mtandao kutoa mafunzo ya biashara, matumizi ya programu za kisasa za biashara, na kupanua matumizi ya teknolojia katika biashara na ujasiriamali. “Hivyo, nitoe rai kwa taasisi za elimu na mafunzo ya biashara kujikita katika matumizi ya teknolojia katika utoaji wa mafunzo”
Pia, ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau waendelee kuimarisha na kuboresha mifumo ya elimu ya biashara katika ngazi zote za shule na vyuo na kuhakikisha inakidhi mahitaji ya soko la ajira.
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Taasisi za elimu na mafunzo ya biashara zihakikishe zinakuza ushirikiano na sekta binafsi ili kusaidia katika kubaini mahitaji halisi ya soko na kutoa mafunzo na elimu inayoendana na mabadiliko ya sekta ya biashara.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema ni muhimu kuhakikisha kuwa biashara si tu zinanufaisha wamiliki, bali pia zinachangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. “Biashara zinapaswa kuchangia katika kulinda mazingira na ustawi wa jamii”.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo amesema kuwa kongamano hilo maalum la kitafiti litasaidia kuibua mijadala itakayowezesha kubaini changamoto na fursa zitazoisaidia nchi kupata mafanikio katika sekta ya biashara na uchumi.
0 Comments