WAZIRI CHANA ASISITIZA MIKAKATI ENDELEVU KUKUZA SEKTA YA UTALII NA UKARIMU

 



Na Happiness Shayo-Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati endelevu katika kukuza Sekta ya Utalii na Ukarimu hususan katika nyanja za utunzaji wa mazingira, ustawi wa jamii, kutumia teknolojia za kidijitali na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa maendeleo endelevu na ustawi wa Sekta ya Utalii.

Ameyasema hayo leo Novemba 21, 2024 wakati akifungua rasmi Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kuunganisha wanataaluma na wadau wa Utalii na Ukarimu katika Nchi Zinazoendelea uliofanyika jijini Arusha.

"Mkutano huu una lengo la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya utalii ambapo kupitia mkutano huu wanataaluma watatoa matokeo ya tafiti na mifumo ya kinadharia inayohitajika kuelewa changamoto kubwa zilizopo, wakati wadau wa sekta watatoa ufahamu wa vitendo kupitia uzoefu wao katika kazi na biashara za utalii ili kusaidia kuleta uvumbuzi, kuimarisha mafunzo, na kuongeza ajira" amesema Mhe. Chana.

Amefafanua kuwa ili Sekta ya Utalii na Ukarimu iendelee ni vyema kukawa na hatua za kulinda mazingira kwa kuhifadhi misitu, wanyamapori, na rasilimali za baharini pamoja na kuwepo na ushirikishwaji wa jamii kwa kuwepo na utalii wa kijamii.

Kuhusu matumizi ya teknolojia ya kidijitali, Mhe. Chana amefafanua kuwa msisitizo juu ya teknolojia katika mkutano huo ni muhimu hasa katika kujadili mada za Mawasiliano ya kidigitali na matumizi ya kompyuta katika Ukarimu na Utalii akitolea mfano kutalii kidigitali na kuwa na vyumba vya hoteli vinavyoendeshwa kidigitali.

Aidha, amesema mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Utalii yanapelekea kufikiria upya kuwa, utalii sio tu njia ya kufikia malengo bali unaambatana na utunzaji wa mazingira na uboreshaji wa jamii.

"Mijadala kuhusu kupunguza athari za mazingira katika Ukarimu na Utalii pia usimamizi wa taka katika upande wa  Ukarimu, zinatoa changamoto ya kufikiria upya namna ilivyofanyiwa kazi na kuhakikisha kwamba Tanzania inapata namna nzuri endelevu itakayosaidia sekta ya Utalii kukua.

Naye,  Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Dkt. Florian Mtey amesema kuwa wakati dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi ni muhimu kuwepo na mijadala endelevu kuhusu namna ya kukabiliana nayo pamoja na namna ya  kukuza utalii na ukarimu kwa kutumia mbinu rafiki wa mazingira, teknolojia za kidijitali, na fursa zingine zilizopo.

Mkutano huo wenye kaulimbiu "Mikakati ya Utalii Endelevu na utalii wa bahari kufikia malengo endelevu na ya kidigitali, yaani “Green and Blue Tourism Strategies Towards Sustainability and Digitalization,” ulioandaliwa na NCT kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane kutoka nchini Afrika Kusini na Chuo cha Utalii cha Kenya kutoka nchini Kenya umehudhuriwa na wadau wa utalii kutoka Kenya, Afrika Kusini, Zambia, Malawi, Botswana, Marekani, Finland, Korea Kusini, India, Sweden, Ethiopia, Ujerumani, China, Uholanzi pamoja na Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii,Wakuu wa Taasisi za Elimu kutoka Nchi mbalimbali, Wawakilishi kutoka Mashirika ya Utalii na Wawakilishi kutoka Vyama vya Usafiri wa Anga Nchini.








Post a Comment

0 Comments