---------------------------
*Na WMJJWM, Iringa*
----------------------------
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, *Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima* ametoa wito kwa wanaume wote nchini kushiriki ipasavyo katika utatuzi wa changamoto za kijamii zikiwemo umasikini, ukatili wa kijinsia na maradhi.
*Dkt. Gwajima* amesema hayo wakati akifungua kongamano la Wanaume lenye lengo la kuongeza kasi ya ushiriki wa Wanaume kukabiliana na changamoto za kijamii lililofanyika tarehe 19 Novemba 2024, katika ukumbi wa kichangani mkoani Iringa.
Amesema tafiti zinaonesha ushiriki mdogo wa wanaume katika kushughulikia masuala ya umasikini, udumavu, ukatili wa kijinsia na malezi ya watoto, hali inayosababisha kushamiri kwa matatizo hayo. Kupitia makongamano, kampeni mbalimbali na juhudi zinazoendelea zitasaidia kuchochea ushiriki wa wanaume na kuimarisha mchango wao katika kutatua changamoto hizo.
"Wanaume kama viongozi wa familia mna jukumu kubwa kushirikiana na wenza wenu ili kujenga familia zenye msingi thabiti. Mna wajibu mkubwa wa kuisaidia jamii kutatua changamoto na hasa kwa kuzingatia nafasi yenu kwenye familia kama viongozi wa taasisi ya familia" amesema *Dkt. Gwajima.*
Naye *Mkuu wa mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba* amewataka wanaume wote kusimama imara katika familia zao na kutimiza wajibu wao kama viongozi wa familia huku akiwaomba kutumia busara zaidi katika kufanya maamuzi kwa kushirikiana na wenza wao na sio kutumia nguvu zinazosabibisha kufanya ukatili ambapo ni kinyume cha Sheria.
Wakizungumza katika kongamano hilo *baadhi ya viongozi wa dini* wamesema kuwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali kama ukatili wa kijinsia, changamoto ya malezi, udumavu na maradhi wanaume wanapaswa kuishi kwa misingi ya kumjua Mungu zaidi kwa sababu Mungu ndiye amewaumba ili kuishi katika mafundisho yake, na wanapaswa kutimiza majukumu yao katika ngazi ya familia na kijamii.
0 Comments