Na Josephine Maxime, Njombe
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mkoani Njombe Mhe. Zakaria Mwansasu amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO kwa kufadhili na kushiriki uendeshwaji wa kampeni ya kupanda miti 50,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mhe. Mwansasu ametoa pongezi hizo leo Februari 6, 2025 alipokuwa akizindua kampeni hiyo iliyowashirikisha Wafanyakazi wa TANESCO,Wafanyakazi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na wananchi katika kata ya Igwachanya kampeni ambayo imelenga kupanda miti 25,000 wilayani humo huku mingine 25,000 ikitarajia kupandwa Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro.
“Niwapongeze TANESCO pamoja na Taasisi ya Waandishi wa Habari za Mazingira. Niwaombe waendelee kuhamasisha na kufanya haya mazoezi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Sisi Wananging’ombe tunajivunia kuwa miongoni mwa wilaya ambazo zinapeleka maji katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere, ” amesema Mhe. Mwansasu.
Amesema Wilaya ya Wanging’ombe ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Njombe ambayo ina vyanzo vingi vya maji vinavyotiririsha maji katika Bwawa la Julius Nyererere ambao hadi kukamilika kwake utazalisha Megawat 2115 hivyo kuchangia upatikanaji wa umeme nchini.
“Kwa umuhimu huo sisi kama Wilaya yenye vyanzo vya maji yananayokwenda kwenye Bwawa, lazima tuongeze jitihada za kutunza mazingira,”alisisitiza Mhe. Mwansasu.
Naye Meneja wa TANESCO Wilayani humo Francis Mvukie amempongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kufadhili mradi huo kwa kuwa manufaa yake yataonekana moja kwa moja hususani katika masuala ya uzalishaji wa umeme.
‘Huu upandaji wa miti ni mahsusi kabisa kwa ajili ya kazi yetu ya kuzalisha umeme,mimi kama Meneja wa TANESCO Wilaya ya Wanging’ombe nampongeza sana, lakini pia naipongeza menejimenti yote ya TANESCO kwa kufadhili mradi huu, ”alifafanua Bw Mvukie.
Kwa Upande wake mhandisi wa Mazingira kutoka TANESCO Makao Makuu, Amina Rajab amesema hatua hii ya upandaji miti ni endelevu na ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya upandaji miti iliyoanzishwa mwaka 2023.
Hadi sasa miti 8000 imeshapandwa katika Wilaya ya Wanging’ombe huku mingine 17,000 ikitarajia kupandwa katika maeneo mbalimbali Wilayani humo.
0 Comments