📌 *Ni kupitia mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Waziri wa Petroli na Gesi Asilia India*
📌 *Gesi, Nishati Safi ya Kupikia na Bayofueli zatajwa*
📌 *India yaipongeza Tanzania usambazaji umeme vijijini*
📌 *Dkt. Biteko akaribisha wawekezaji,wafanyabiashara kutoka India*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh kuhusu nia ya nchi hiyo kuzidi kuimarisha biashara kati yake na Tanzania kupitia sekta binafsi, kufanya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati na kujengea uwezo wataalam.
Mazungumzo hayo yamefanyika Februari 11, 2025 jijini New Delhi nchini India katika Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati nchini humo.
Dkt. Doto Biteko amemweleza Waziri Singh kuwa milango ya uwekezaji Tanzania ipo wazi na kampuni mbalimbali kutoka India zinaweza kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya umeme, usambazaji wa gesi ya mitungi (LPG) na uagizaji wa mafuta kwa pamoja (Bulk procurement) kwani kunahitajika washindani wengi ambao watatoa uhakika wa uwepo wa mafuta wakati wote.
“ Tanzania tumejikita katika kuhakikisha tunatumia kila rasilimali tuliyonayo ili kuwa na nishati ya kutosha ikiwemo umeme ili kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ameeleza kuhusu umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza miradi mbalimbali akitolea mfano kuwa, ili Tanzania ijitosheleza kwa mahitaji ya nishati inahitaji Dola za Marekani Bilioni 12 ambazo kupatikana kwake lazima sekta binafsi ihusishwe hivyo kupitia kwa Waziri Singh, amekaribisha wawekezaji kutoka India kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati nchini.
Kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Nishati India amesema kuwa Tanzania imefaidika na ushiriki wake katika Wiki hiyo kwani India tayari imeshapiga hatua kwenye Sekta ya Nishati hivyo imekuwa ni sehemu maalum ya kujifunza zaidi kuhusu sekta, kubadilishana uzoefu na kunadi fursa za uwekezaji ikiwemo duru ya tano ya uendelezaji wa visima vya mafuta na gesi asilia Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh amesema kuwa India ina uhusiano mzuri wa kibiashara na Tanzania ambapo biashara kati ya pande hizo mbili imezidi kuimarika na kueleza kuwa nchi hiyo imejipanga kuimarisha zaidi biashara yake kwa Tanzania.
Ameeleza kuwa, nchi hiyo pia kupitia Sekta binafsi inataka kuwekeza kwenye usambazaji wa mitungi ya gesi nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia huku akieleza kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kwa kusambaza mitungi ya gesi kwa asilimia 99.9 kwa wananchi wake.
Ameongeza kuwa India imeamua kuwekeza kwenye uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia ambapo baadhi ya kampuni zake zimejitokeza kushiriki Duru la Tano la kunadi vitalu vya Mafuta na Gesi Asilia linalotarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi Machi nchini.
“ India pia tupo tayari kuwekeza kwenye gesi ya kusindika (LNG), bayofueli pamoja na kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kitaalam yanayohusu Sekta ya Nishati kwa kuwajengea uwezo zaidi wataalam wa Tanzania na pia kuwa na programu ya kubadilishana wataalam kati ya Tanzania na India,” asema Mhe. Singh
Pia, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kwenye usambazaji wa umeme hususan vijijini na kwa jinsi inavyotekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa namna mbalimbali ikiwemo kuweka ruzuku kwenye mitungi ya gesi.
Vilevile, Waziri Singh amempongeza pia Dkt. Biteko kwa hekima zake na ukomavu ambao anauonesha pale anapoieleza dunia kuhusu masuala ya uendelezaji wa rasilimali zinazoweza kuzalisha umeme ambazo Bara la Afrika imebarikiwa nazo lakini mpaka sasa hazijaendelezwa ipasavyo kutokana na misimamo ya kidunia ikiwemo makaa ya mawe ambayo yakiendelezwa yatazidi kutoa uhakika wa uwepo wa nishati ya kutosha.
Mazungumzo kati ya viongozi hao yamehudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye anamwakilisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Idd Kassim, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile.
0 Comments