UTAPELI WA MTANDAONI UMEPUNGUA KWA ASILIMIA 19: WAZIRI SILAA

 





Na mwandishi wetu

Serikali imefanikiwa kupunguza matukio ya utapeli wa mtandaoni kwa asilimia 19 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinazopatikana katika ukurasa wa 40 wa taarifa ya robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) leo Januari 31, 2025 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu maswali ya Mhe. Tulia Ackson (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Angelina Mabula (Mb), Mbunge wa Ilemela kuhusu kushamiri kwa matukio ya uhalifu mtandaoni na majina ya viongozi kutumika kufanya utapeli huo.

Mhe. Silaa amesema kuwa hatua kadhaa zimeshachukuliwa na Serikali ili kupunguza utapeli mtandaoni ikiwa ni pamoja na Wizara yake kuratibu kikao cha kimkakati cha kisekta kilichofanyika tarehe 22 Novemba, 2024 ambapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; Jeshi la Polisi; Makampuni ya simu na wadau wengine walishiriki.

“Kikao hicho kimezaa kikosi kazi cha wataalamu ambao wameshaanza kazi hivi ninavyozungumza na tumekubaliana na Mhe. Bashungwa mapema mwezi Februari 2025 tutakaa kikao tena cha viongozi wa juu kuangalia njia za kufanya, kubwa tuliloelekeza kampuni za simu ni kutoa elimu kwasababu ukiangalia utapeli wa aina zote una ulaghai ndani yake”, amesema Waziri Silaa.

Katika hatua nyingine Mhe. Silaa amewataka watanzania kuhakikisha hawabonyezi link ambazo wanatumiwa kuambiwa wameshinda bahati nasibu, au kuna mkopo wa Spika au wa kiongozi mwingine. Jambo la pili amesisitiza wananchi wasitoe namba zao za siri kwa mtu yeyote, na tatu ameelekeza makampuni ya simu kuendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa umma.

“Serikali itaendelea kufanya kazi ya kuhakikisha inasaidia wananchi dhidi ya uhalifu huu na Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi liliahidi kufanya operesheni hasa kwa Mikoa ya Rukwa na Morogoro ambayo ina matukio mengi kwa mujibu wa takwimu za TCRA”, alisisitiza Waziri Silaa.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Mhe. Tulia Ackson (Mb) aliwataka wabunge kama wawakilishi wa wananchi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano na kujiepusha na ulaghai wa mtandaoni kwani hakuna fedha za bure.

Sambamba na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amejibu swali la Mhe. Festo Sanga (Mb) kuhusu usajili wa simu kiholela zinazotumika kufanya utapeli amesema kuwa Serikali imechukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kutoa namba *106# ya huhakiki taarifa za usajili wa laini za zimu na namba 15040 ya kuripoti matukio ya uhalifu kwa njia ya simu.

Post a Comment

0 Comments