TEF YAWATAKA WANAHABARI KUVAA VITAMBULISHO NA REFRACTOR WAKATI WA KUSIKILIZA KESI MAHAKAMANI

 




Na mwandishi wetu

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kupitia kwa Mwenyekiti wake Deudatus Balile, limeelezea masikitiko yake kufuatia tukio la kuzuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao wakati wa usikilizwaji wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Balile amesema kuwa kitendo cha kuwazuia wanahabari kukusanya taarifa ni kuvunja haki yao ya kikatiba, ambayo inawalazimu kukusanya na kusambaza habari kwa umma. Hata hivyo, amesema TEF haikuona busara ya kutoa tamko kwa haraka, bali waliona ni vyema kukutana na Jeshi la Polisi ili kuzungumza na kutafuta suluhu ya kudumu.

Katika mazungumzo hayo, TEF na Jeshi la Polisi wamekubaliana kuwa siku ya Jumatatu, tarehe 6 Mei 2025 ambapo kesi itaendelea kusikilizwa hivyo waandishi wa habari wote wataruhusiwa kuingia mahakamani, kwa masharti kwamba kila mmoja awe na kitambulisho cha kazi au jaketi maalum la utambulisho.

“Ni lazima tuwe na utambulisho sahihi,” amesema Balile. “Hata katika maeneo ya migogoro au vita, waandishi huruhusiwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata taratibu maalum. Sisi pia tunapaswa kufanya hivyo.”

Balile pia ametoa wito kwa waandishi kuwahi eneo la tukio, kuvaa mavazi rasmi yanayoendana na mazingira ya mahakama, na kuzingatia maadili ya taaluma yao. Aidha, amesisitiza kuwa hata maafisa habari wa vyama vya siasa wanapaswa kuwa na vitambulisho rasmi ikiwa watahitaji kupata taarifa.

"Kwa yeyote atakayekumbana na tatizo lolote siku hiyo, anatakiwa kuwasiliana na ofisi ya TEF au uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Jiji la Dar es Salaam (DPC). amesisitiza Balile.

Kwa upande wake, Bakari Kimwaga, Mwenyekiti wa DPC, amesema wao kwa kushirikiana na TEF waliamua kuwa na subira na kutafuta majadiliano badala ya kutoa matamko ya papo kwa papo. Amewashauri waandishi wa habari kuweka mbele usalama wao na kufanya kazi kwa kufuata kanuni na miongozo ya taaluma, wakiepuka uandishi wa kiharakati.

Post a Comment

0 Comments