Mkuranga, Pwani – Julai 20, 2025
Taarifa kutoka Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani zinaeleza kuwa hali ya sintofahamu imetanda baada ya wananchi kukamata kura feki zilizodaiwa kuwa tayari zimepigwa katika uchaguzi wa awali wa ndani wa chama kwa nafasi za madiwani.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo ukumbini, kura hizo feki zilinaswa kabla ya kuingizwa rasmi katika sanduku la kura. Inadaiwa kuwa baadhi ya wajumbe waligundua kuwa kuna idadi kubwa ya karatasi za kura ambazo tayari zilikuwa zimepigwa kabla ya zoezi rasmi la upigaji kura kuanza.
Tuhuma nzito zimeelekezwa kwa Katibu wa Chama Wilaya pamoja na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) ambao wanadaiwa kuhusika kuingiza kura hizo ukumbini. Wananchi waliokuwepo walichukua hatua ya kuzizuia na kulazimika kusimamisha kwa muda mchakato wa uchaguzi huo.
Baadhi ya wagombea waliokuwepo wameeleza kusikitishwa kwao na kitendo hicho wakikitaja kama hujuma inayolenga kuvuruga mchakato wa haki na uwazi ndani ya chama.
Mpaka sasa haijafahamika iwapo vyombo vya dola vimehusika kuanza uchunguzi rasmi juu ya tukio hilo, ingawa sauti za kutaka viongozi waliotajwa kuchukuliwa hatua kali zimeanza kusikika kutoka kwa wanachama walioguswa.
Taarifa zaidi juu ya hatua zitakazochukuliwa na uongozi wa chama katika ngazi ya mkoa au taifa bado hazijatolewa rasmi.
0 Comments