‎WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA KUWA MGENI RASMI MAONESHO YA HUDUMA ZA KIFEDHA NA KIJAMII 'MUHARRAM EXPO' ‎




 


‎Na Madina Mohammed Dar es Salaam

‎Waziri wa Viwanda na Biashara, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Pili ya Huduma za Kifedha na Kijamii 'Muharram Expo' yanayoendelea katika viwanja vya wazi vya jiji la Dar es Salaam. Maonesho haya, yanayoanza Jumatatu hii, ni sehemu ya sherehe za kuingia mwaka mpya wa Kiislamu, Muharram, na yamejumuisha shughuli za kifedha zinazozingatia misingi ya kisheria ya Kiislamu, hususan huduma zisizo na riba.

‎Kwa mujibu wa Kiongozi Mwandamizi wa Taasisi za Kiislamu nchini, Mohamed Issa, maonesho haya ni fursa ya kipekee kwa Watanzania kujifunza kuhusu huduma za kifedha zinazozingatia maadili ya Kiislamu. "Maonesho haya yameanza Jumanne hii na ni ishara muhimu ya kuingia kwa mwaka mpya wa Kiislamu. Tunatarajia kuwa wananchi watapata elimu ya muhimu kuhusu huduma za kifedha zisizo za riba, ikiwemo huduma za kibenki, vicoba, na Saccos," alisema Issa.

‎Katika maonesho haya, wananchi watapata fursa ya kujifunza jinsi ya kuwekeza na kupata mikopo au msaada wa kifedha pasipo kutumia riba, kwa mujibu wa Shari'ah. Vilevile, maonesho hayo yatawasilisha mifuko ya Uwekezaji Halal, mifuko ya pamoja ya uwekezaji (Collective Investment Schemes), na huduma za masoko ya mitaji na dhamana. Watapata pia elimu kuhusu sukuk, hati fungani zisizo na riba, ambazo zimejizolea umaarufu kwa kuwa ni njia sahihi za uwekezaji zinazoendana na misingi ya Kiislamu.

‎Issa alieleza kuwa wananchi watapata elimu muhimu kuhusu hisa za kampuni zinazokidhi masharti ya Shari'ah, pamoja na jinsi ya kuepuka hisa zinazozingatia riba au zile zisizo Halal. "Tunataka jamii iwe na uelewa wa kina kuhusu uchumi wa Kiislamu, ili kila Mtanzania aweze kufanya maamuzi bora kuhusu fedha zao," aliongeza.

‎Mbali na huduma za kifedha, maonesho haya pia yatatoa elimu kuhusu masuala ya kijamii kama vile uwekaji wa wakfu, huduma za afya, na msaada wa kisheria. Madaktari watawawepo kutoa huduma za afya bure kwa wananchi, na kutakuwa na uchangiaji wa damu, huduma muhimu kwa afya ya jamii. Huu ni mfano mzuri wa jinsi huduma za kijamii zinavyoweza kuunganishwa na shughuli za kifedha ili kuboresha maisha ya Watanzania.

‎"Katika maonesho haya, tunatoa elimu kuhusu masuala ya uchumi na fedha, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa ushirikiano katika jamii, hasa kwa wafanyabiashara ambao wanakutana na changamoto za mikopo. Tunalenga kuwasaidia watu kutatua matatizo yao kwa njia ya elimu sahihi," alisema Issa.

‎Naye Amiri wa Baraza Kuu la Kiislamu, Sheikh Mussa Kundecha, alisisitiza kuwa maonesho haya hayahusishi waislamu pekee bali ni kwa Watanzania wote, bila kujali dini au imani zao. "Maonesho haya yameandaliwa kwa ajili ya Watanzania wote. Lengo letu ni kuelimisha na kutoa huduma kwa wananchi wote, hususan wafanyabiashara, ili kuwasaidia kuepuka madhara ya mikopo isiyozingatia maadili," alisema Sheikh Kundecha.

‎Sheikh huyo aliongeza kuwa, ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anafaidika na maonesho haya, shughuli hizo zimeandaliwa katika viwanja vya wazi ili kuwa na ufikiaji wa urahisi kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji.

‎Mada nyingine zitakazowasilishwa kwenye maonesho hayo ni kuhusu madhara ya riba katika jamii na uchumi wa Kiislamu. Kwa miongo kadhaa, riba imekuwa ikichukuliwa kama kipingamizi cha maendeleo ya uchumi na jamii, na katika maonesho haya, wataalam wa fedha na uchumi watazungumzia jinsi gani riba inavyoweza kudumaza ukuaji wa biashara na kujenga mzunguko wa fedha usio endelevu.

‎Maonesho ya Huduma za Kifedha na Kijamii 'Muharram Expo' yanatoa fursa ya kipekee kwa Watanzania kujifunza na kufahamu masuala ya kifedha yanayozingatia maadili ya Kiislamu, huku pia yakitoa huduma muhimu za kijamii kama afya na msaada wa kisheria. Hii ni fursa kwa kila Mtanzania kuwa na elimu ya kutosha kuhusu njia bora za kutumia rasilimali zao bila kuvunja sheria za dini.

Post a Comment

0 Comments