JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU
NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI
WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO,
TAREHE 2 MEI, 2016
Ndugu wanahabari,
Ni miezi minane sasa imepita tangu mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu uanze nchini, ambapo wizara
yangu imekuwa ikitoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huu kila wiki, na kufanya majumuisho kila mwezi,
ili kutoa tahadhari kwa wananchi na maelekezo ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na mlipuko huu. Kwa
mara nyingine tena, ninatoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa wa Kipindupindu, ikiwa ni ya mwisho wa
mwezi wa nne mwaka huu wa 2016. Takwimu zinaonyesha kuwa, hadi kufikia tarehe 1 Mei 2016, jumla ya
wagonjwa 21,124 wametolewa taarifa na kati ya hao 331 wamepoteza maisha. Ni mikoa ya Njombe na
Ruvuma tu ambayo haijaripoti mgonjwa yeyote wa Kipindupindu tangu mlipuko huu uanze mnamo mwezi
Agosti mwaka 2015.
Ndugu wanahabari,
Ninapenda kusema kuwa, hivi sasa kuna mabadiliko chanya katika mwenendo wa Kipindupindu, ambapo
ugonjwa huu sasa unapungua katika maeneo mengi nchini, jambo ambalo linatia moyo sana. Takwimu za
mwezi wa Aprili 2016 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa 1,037, idadi ambayo ni sawa na punguzo
la asilimia 65 kutoka wagonjwa 2,953 walioripotiwa mwezi Machi 2016. Katika mwezi huu wa Aprili 2016,
idadi ya wagonjwa imekuwa ikipungua kila wiki kutoka 368 wiki ya kwanza, 212 wiki ya pili, 143 wiki ya tatu
hadi 104 wiki ya nne. Mikoa iliyoongoza kuwa na wagonjwa wapya wengi zaidi mwezi Aprili ni Mara (270),
Kilimanjaro (198), Morogoro (188) na Dar-es-Salaam (90). Idadi ya vifo vilivyoripotiwa mwezi Aprili ni 16,
wakati vifo vilivyoripotiwa mwezi Machi vilikuwa 47. Idadi hii ya vifo ni pungufu kutoka asilimia 1.6 ya
waliougua mwezi Machi hadi asilimia 1.5 ya waliougua mwezi Aprili.
2
Ndugu wanahabari,
Licha ya kuwa na mwenendo chanya katika kasi ya kupungua kwa ugonjwa huu, bado kuna mikoa
inayohitaji kuongeza juhudi zaidi katika mapambano haya. Mikoa hii ni Morogoro, Kilimanjaro, Mara, Pwani
na Dar-es-Salaam, ambapo ugonjwa huu umedumu kwa muda mrefu zaidi. Katika mikoa hii, tutaendelea ku
peleka timu kutoka ngazi ya Taifa kwa ajili ya kushirikiana na timu zilizopo mkoani na wilayani ili kuongeza
nguvu zaidi katika kukabiliana na tatizo hili.
Ndugu wanahabari,
Wizara ninapenda kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
Hata hivyo, ninaendelea kusisitiza kuwa, pamoja na kuwa takwimu zinaonyesha ugonjwa kuendelea
kupungua, bado hali si salama. Hali ya hewa iliyopo sasa katika maeneo mengi nchini inasababisha tuwe
na wasiwasi zaidi, kwani mvua za masika pamoja na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa watu kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za usafiri na za biashara, bado ni tishio katika kusambaa au kuibuka upya kwa
ugonjwa. Kwa kuwa hakuna mkoa wowote ambao upo salama katika kuibuka upya kwa ugonjwa huu,
bado Wizara inaendelea kusisitiza kuwa hatua za tahadhari ziendelee kuchukuliwa ili kuzuia maambukizi,
na pia taarifa za ugonjwa ziendelee kutolewa kila siku, hata kama hakuna mgonjwa yeyote.
Ndugu wanahabari,
Wizara yangu inatoa onyo kali kwa Wasimamizi wa huduma za Afya Mikoani na katika Halmashauri,
ambao wanaficha taarifa za wagonjwa wa Kipindupindu. Yeyote atakayebainika kuwa anaficha taarifa hizi
atachukuliwa hatua kali. Wizara yangu inasisitiza kuwa, juhudi za kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali
za udhibiti wa mlipuko huu ziendelee. Katika kipindi hiki ambapo ugonjwa unaendelea kupungua,
Wasimamizi wa huduma za Afya Mikoani na katika Halmashauri, waendelee kufuatilia na kuchunguza kwa
kina, taarifa zote za vifo vinavyotokana na mgonjwa mwenye dalili za Kipindupindu kama kuharisha na
kutapika. Taarifa hizi zinahitajika ili hatua madhubuti za kuzuia vifo ziweze kuchukuliwa.
Ndugu wanahabari,
Wizara inasisitiza kwamba kila jitihada zifanyike kote nchini ili kuhakikisha kuwa jamii yote ya Watanzania
inatumia maji safi na salama. Ninaendelea kutoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi
na usafi wa mazingira. Katika kipindi hiki cha mvua za masika, utiririshaji ovyo wa maji taka ni marufuku,
na mamlaka husika katika ngazi za vitongoji, vijiji, kata na tarafa zichukue hatua za kisheria kwa wale
wote watakaobainika kufanya jambo hili.
Ndugu wanahabari,
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana
na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
Utoaji na upatikanaji wa takwimu sahihi za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na
Wizara, na bila kuingiliwa na viongozi wa kisiasa au kiserikali.
Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo yote ya mijini na vijijini ili kupunguza hatari ya kuenea
kwa ugonjwa huu,
3
Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kupitia Mamlaka za maji zilizopo katika ngazi zote
nchini,
Kuhakikisha upatikanaji wa ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii
iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa
tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
Kuhakikisha utunzaji salama wa maji ya kunywa yaliyotibiwa,
Kufikisha wagonjwa wa Kipindu pindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata
matibabu,
Kuhakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya ORS katika maeneo mbali mbali nchini ili kupunguza
athari za ugonjwa
Ndugu wanahabari,
Wizara yangu pia inatoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa ambao bado haujatambulika ulioripotiwa tarehe
23 Aprili katika mkoa wa Kigoma. Hadi kufikia tarehe 29 Aprili 2016, Jumla ya Wagonjwa 1467 wenye dalili
za homa, kuumwa kichwa, kulegea mwili, maumivu ya viungo, maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika na
kizunguzungu walipatikana katika vijiji vya Songambele, Buhigwe na Mulele katika halmashauri ya wilaya
ya Buhigwe. Hadi sasa kijiji cha Songambele ndicho kimeripoti wagonjwa wengi zaidi (asilimia 68%).
Matibabu yanaendelea kufanyika kwa wagonjwa wote na hakuna kifo kilichoripotiwa hadi sasa. Uchunguzi
bado unaendelea kufanyika na timu ya wataalam wa kufuatilia mlipuko huu imeshaenda mkoani Kigoma
kwa ajili ya ufuatiliaji. Wizara yangu itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa mlipuko huu.
Hitimisho
Wizara inawapongeza na kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na
katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara ili kuutokomeza ugonjwa huu, ikiwa ni
pamoja na wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri
pamoja na waandishi wa habari n a wananchi kwa ujumla.
Asanteni sana
0 Comments