📌📍 *Mkurugenzi wa Kampuni ya Green Hippo Travels azuru Makuyuni Wildlife Park*
📍 *Astaajabishwa na wingi wa vivutio na kuahidi kuwahamasisha wageni mbalimbali kutembelea eneo hilo*
Mkurugenzi wa Kampuni mashuhuri ya utalii inayofahamika kama Green Hippo Travels, Astrid Kleinveld akiwa ameambatana na rafiki yake Naomi Rugenbrink ambao wote ni raia wa Uholanzi, tarehe 15 septemba 2024, walitembelea eneo la Makuyuni Wildlife Park liliopo wilayani Monduli mkoani Arusha kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo na kupata fursa ya kufahamu namna wanavyoweza kufanya biashara ya utalii katika eneo hili hasa utalii wa Kupanda Mlima na Kutembea kwa miguu.
Bi Astrid na mwenzake wakiongozwa na Afisa Utalii wa eneo hilo Chacha Masase walipata fursa ya kupanda Mlima Kipara ambao unapatikana ndani ya eneo hilo wenye urefu wa mita 1900 kutoka usawa wa bahari pamoja na kufanya utalii wa Kutembea kwa miguu hivyo kufanikiwa kuona wanyamapori kwa ukaribu zaidi na kufurahia mandhari iliyopo.
"Uzuri wa eneo hili ni wa kustaajabisha mnoo, tumepata uzoefu wa kipekee ambao nina imani sio sisi tu bali mtalii yeyote atakae kuja ataifurahia Makuyuni Wildlife Park kuanzia mapokezi ya wanyamapori tokea njiani, mandhari ya eneo hili, pamoja na ukarimu na umahiiri wa watumishi wa TAWA" alisema Astrid
" Tumepanda mlima na kutembea kwa miguu tumejionea vivutio vingi ambavyo sasa tunakwenda kuongeza kwenye safari zetu na kuwaalika wageni kutoka pembe zote za dunia kuja kulitembelea eneo hili" aliongeza na kusisitiza.
Uwepo wa miundombinu wezeshi ya barabara, wingi wa wanyamapori na mandhari ya kuvutia huifanya Makuyuni Wildlife Park kuwa chaguo bora kwa mtalii yeyote wa ndani na nje ya Tanzania.
Shughuli nyingine za kitalii zinazoweza kufanyika katika eneo hilo ambalo ni makazi ya wanyamapori mbalimbali wakiwemo Nyati, Simba, Tembo, Chui, Twiga, Pundamilia ni pamoja na kupanda mlima (Hiking), utalii wa kutembea kwa miguu (Walking Safari),Utalii wa kuona ndege, kuangalia jua likichomoza na kuzama na utalii wa Utamaduni (jamii ya kabila la wamasai inayozunguka eneo hili).
0 Comments