MWAROBAINI WA CHANGAMOTO YA MAJI KIBONDO WAPATIKANA

 



*📌 Tanki la Lita 1,500,000 Lajengwa*


*📌 Dkt. Biteko Awataka Wananchi Kigoma Kutunza Vyanzo vya Maji*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Mwaka 2022/23 Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Kibondo ilitenga zaidi ya Shilingi Bilioni 1.49 kwa ajili ya ujenzi wa tanki la maji la ujazo wa lita 1,500,000 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Utekelezaji wa mradi huo unaolenga kutatua changamoto ya maji wilayani Kibondo na kuwawezesha wananchi kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi

Akizungumza leo Septemba 18, 2024 wilayani Kibondo mkoani Kigoma mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tanki hilo, Dkt. Biteko amesema mradi huo wa maji unaojengwa na wataalam kwa kuwashirikisha vijana wa Kitanzania utasaidia kuounguza mgao na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa siku huku akiwataka wananchi wa Kigoma kulinda vyanzo vya maji.

“ Awali maji yalikuwa machache na yenye tope kwa sababu ya kutokuwa na chujio, nataka niwaombe mnavyo vyanzo vya maji mvilinde, mkikata miti hovyo na kuchoma mashamba itasababisha ukame licha ya kuwa na tanki hili mvilinde vyanzo vya maji ili tupate maji kwa muda mrefu,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ametaja faida  za mradi huo kuwa ni kuboresha huduma ya maji kwa kuongeza saa za upatikanaji maji kutoka saa nne hadi 12 kwa siku

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewataka wananchi wa Kigoma kushikamana na kujiepusha na migogoro na badala yake washirikiane ili kuendelea kujiletea maendeleo.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya uendelezaji wa miradi na miundombinu ya maendeleo Mkoani Kigoma.

Amesema fedha hizo ni pamoja na ujenzi wa kwa kiwanda cha kuunda meli ambacho hakipo popote Afrika Mashariki na kati,

Amesema kuwa Meli ya Mv Liemba tayari imetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati na baada ya hapo itaendelea kufanya kazi na biashara kati ya Tanzania, Burundi na DRC Kongo.

“Tutaendelea kusimamia kila fedha ya miradi ambayo itaelekezwa mkoani kwetu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Kigoma.” Amemalizia Mkuu huyo wa Mkoa.

Naye, Mbunge wa Kibondo Mjini, Mhe. Dkt. Florence Saminzi amesema kuwa Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika Jimbo la Muhambwe

“ Katika kipindi cha Rais Samia kumekuwa na maendeleo mbalimbali, tumepata shule tatu mpya za msingi pia tumeboresha madarasa, vyumba vya walimu pamoja na kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya,” amesema Dkt. Saminzi.





Post a Comment

0 Comments