Familia ya Marehemu Mahmoud Ally Hamad Bwato inamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati na kusaidia kutatua mgogoro wa ardhi ambao umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 27.
Mgogoro huo unahusiana na kiwanja Na.186039/95, Plot Na.20 kilichopo Kinondoni Ada Estate, karibu na Leaders Club jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 25, 2024, msemaji wa familia na msimamizi wa mirathi, Hassan Mahmoud Bwato, alisema kuwa familia imekosa hati ya kumiliki kiwanja hicho licha ya maamuzi ya viongozi wa serikali, ikiwemo uamuzi wa mwaka 2018 uliosema hati irejeshwe kwa familia ya Marehemu Mahmoud.
“Tunamwomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka yako kutusaidia kurejeshewa haki yetu ya kumiliki kiwanja hiki ili tuweze kumaliza mgogoro huu wa miaka mingi,” alisema Hassan. “Tumepitia maumivu makubwa ya kiuchumi na kijamii kutokana na mgogoro huu, na tunatarajia msaada wako wa kutatua hali hii.”
Mgogoro huu wa ardhi ulianza mwaka 1997 baada ya kifo cha mzee wao, Mahmoud Ally Hamad Bwato, ambapo baada ya msiba familia ilianza mchakato wa mirathi. Ndipo akajitokeza Mohamed Ikbar Haji, maarufu kwa jina la "Bagdad," alijitambulisha kwao kama mtu anayesaidia yatima na wajane kupitia kampuni yake ya Waqfu Developments na Lavender Villas Ltd. Alidai kuwa angeweza kuwasaidia katika mchakato wa mirathi na kubadilisha umiliki wa hati kutoka kwa marehemu baba yao na kuja kwa familia waliobakia.
Familia ilimpa ushirikiano mkubwa, wakimkabidhi hati ya mauziano ya kiwanja hicho, kibali cha ujenzi, ramani ya nyumba, cheti cha kifo cha mzee wao, na cheti cha mirathi ili apate kumsaidia katika mchakato wa kisheria. Hata hivyo, Mohamed Ikbar Haji aligeuka kuwa tapeli. Aliwapora hati muhimu kutoka kwa familia na akaanza kutekeleza mpango wake wa kuiba kiwanja hicho kwa kudai kuwa aliinunua kwa mnada.
Hadi leo, mgogoro huu umeendelea kuwaathiri familia hiyo kwa kiasi kikubwa. Hati ya kiwanja hicho haijarejeshwa, licha ya maamuzi ya serikali. Familia imekuwa ikiteseka kifamilia, kiuchumi, na kijamii kutokana na uharibifu wa haki yao ya kumiliki mali hiyo.
Mnamo Agosti 24, 2018, maamuzi yalifikiwa na Mohamed Ikbar Haji alitakiwa kuwasilisha hati ya kiwanja hicho kwa familia ili kumaliza mchakato wa kurejesha haki ya umiliki. Hata hivyo, tangu wakati huo, hati hiyo haijarejeshwa kwa familia.
Akielezea madhara yaliyosababishwa na mgogoro huu, Hassan Mahmoud Bwato alisema, walifukuzwa kutoka kwenye nyumba yao na kulazimika kuishi nje kwenye kibanda cha mabati mpaka pale Mkuu wa wilaya ya Kinondoni wa kipindi cha miaka ya hivi karibuni Ally happy kuwasaidia kuwaondosha wanyang'anyi hao waliogeuza nyumba yao kuwa moja wapo ya ofisi za kampuni ya Tapeli huyo.
"Mateso ambayo familia yetu imepata kutokana na mgogoro huu ni. makubwa sana. Walishindwa kuendelea na masomo yao kutokana na changamoto zilizozunguka familia, na baadhi yao walilazimika kuacha shule kabisa. Pia, sisi kama familia tulikosa amani, tukawa katika hofu ya kupoteza mali yetu, hali iliyoleta magonjwa ya shinikizo la damu kwa baadhi ya wazazi wetu."
0 Comments