Na mwandishi wetu
Leo Septemba 19, 2024 aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Tume, CPA. William Mtinya amekabidhi Ofisi kwa Nsajigwa Kabigi aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara ya Afya.
Akizungumza kwenye ofisi za makao makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma mbele ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Tume, CPA William Mtinya ameshukuru watendaji wa Tume ya Madini kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha tangu aliposhika nafasi hiyo na kuwataka kuendelea kumpa ushirikiano Kaimu Mkurugenzi mpya wa Huduma za Tume.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mpya wa Huduma za Tume, Nsajigwa Kabigi ameomba watumishi wote wa Tume ya Madini kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.
Amesisitiza kuwa Ofisi yake itaendelea kutatua changamoto mbalimbali sambamba na kuboresha mazingira ya ofisi zote za madini nchini kwa kuhakikisha zinapata vitendea kazi ili kutoa huduma za uhakika kwa wadau wa madini waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Wakati huohuo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo sambamba na kuwataka watumishi kuendelea kumpa ushirikiano Mkurugenzi mpya wa Huduma za Tume amewataka kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu na kufuata sheria kwa kuwa watanzania wengi bado wana matarajio makubwa kutoka Sekta ya Madini.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuainisha fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini ili kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini ili kuendana na Vision 2030 ya “Madini ni Maisha na Utajiri.”
0 Comments