Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 25, 2024, RC Chalamila amesema kuwa zoezi la upigaji kura litaanza saa 2:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni.
Amehimiza wakazi wa Dar es Salaam kufuata taratibu zote za uchaguzi ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka, huku akiwataka wananchi kufika mapema katika vituo vya kupigia kura na kuhakikisha kuwa wanafuata miongozo ya uchaguzi, akisisitiza kuwa mtu yeyote atakayefika kituoni baada ya saa 10:00 jioni hataruhusiwa kupiga kura isipokuwa wale walio kwenye mstari.
"Ni muhimu wananchi kuzingatia taratibu na miongozo ya uchaguzi ili watimize haki yao ya kikatiba. Wale watakaochelewa baada ya saa 10:00 jioni, hawataruhusiwa kupiga kura," alisema RC Chalamila.
Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa utahusisha wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18. Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kuwa na jumla ya mitaa 564, ambapo kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni, mkoa huu una watu zaidi ya milioni 5.3, na takribani milioni 3 kati yao wanatarajiwa kuwa na umri wa kupiga kura.
RC Chalamila alikumbusha kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu kwa kuimarisha demokrasia na kujenga utawala bora, ambapo wananchi watachagua wenyeviti na wajumbe wa mitaa, vijiji, na vitongoji. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kutoa haki yao ya kikatiba na kuchagua viongozi wanaowafaa.
Akiwahimiza wapenzi wa vyama mbalimbali, RC Chalamila alisema kuwa uchaguzi huu utatoa nafasi ya kudumisha demokrasia na amani, huku akiwashauri wananchi kuchagua viongozi bora ambao watasaidia kukuza maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
"Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa uchaguzi huru na haki, na tunapaswa kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unafuata misingi ya demokrasia na unajali maslahi ya wananchi," alisema RC Chalamila.
Pia alitolea ufafanuzi kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kuhusu upungufu wa taarifa na maandalizi ya uchaguzi, akisisitiza kuwa uchaguzi unapaswa kuwa wa uwazi na haki, na kwamba mkoa wa Dar es Salaam umejizatiti katika kuhakikisha usalama na urahisi wa upigaji kura kwa wananchi.
Aidha RC Chalamila amesisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kila raia, na kila Mtanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anapaswa kutumia haki hiyo.
0 Comments