Na OR TAMISEMI, Arusha
Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlota Marcias amesema Serikali ya Sweden itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo katika kuendeleza elimu kwa kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali zinazoonekana kwenye Sekta ya Elimu nchini.
Mhe. Charlota Marcias ameyasema hayo Jijini Arusha Novemba 20, 2024 katika Shule ya Msingi Muriet Darajani iliyopo Jijini Arusha mkoani Arusha na kusisitiza kuwa urithi mkubwa wa Watoto ni elimu na ndiyo maana Sweden inaendelea kuunga mkono jitihada za utoaji elimu nchini kwenye miradi ya elimu hususani miradi ya GPE na Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
Aidha, Mhe. Charlota amesema kwa sasa kipaumbele kikubwa ni kuboresha eneo la ufundishaji na ujifunzaji wa walimu na wanafunzi kwenye maeneo ya utoaji wa vitabu, Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA) na ujenzi wa miundombinu ambayo itawafanya walimu waweze kuboresha utoaji wao wa elimu kwa wanafunzi hapa nchini.
Akiongea kwa niaba ya Serikali Dkt. Mahera Wilson Charles, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha Sekta ya Elimu kusonga mbele kwa kujenga miundombinu mipya na kutoa vitabu ambavyo vimeboresha uwiano kati ya wanafunzi na vitabu kote nchini.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muriet Darajani Dominick Gado amesema shule yake ilipokea Shilingi 55,824,000 zilizojenga madarasa mawili ya mfano na samani zake, kuweka bembea, ununuzi wa vifaa vya michezo kwa ajili ya Watoto wa awali, matundu sita ya vyoo na tenki la maji safi lakini pia kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) shule yake ilipokea Shilingi 108,800,000 ambazo zilijenga vyumba vitano vya madarasa ambavyo vimepunguza msongamano shuleni hapo.
Ziara hiyo ya kikazi ya siku nne kati ya Serikali na Ubalozi wa Sweden inalenga kuangalia ufanisi wa Mradi wa GPE LANES II na Programu ya EP4R kwenye mikoa ya Arusha na Mara.
0 Comments