TUMEPATA SOMO LA KUCHUNGUZA USALAMA WA MAGHOROFA YA KARIAKOO - Mhe. Dkt. Samia

 



Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu amesema tukio la kuanguka jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Mchikichi na Manyema uliopo Kariakoo jijini Dar es Salaam, limetoa somo kwa Serikali kuanza uchunguzi wa kuhakikisha kunakuwa na usalama wa binadamu na mali zao kwenye magorofa yaliyojengwa Kariakoo.

Mhe. Rais amesema hayo Kariakoo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kulitembelea jengo hilo lililoanguka Novemba 16, 2024 na kupewa taarifa kuwa jengo hilo limesababisha vifo vya watu 20.

“Tukio hili limetupa somo kubwa la kuangalia usalama wa majengo yetu katika eneo la Kariakoo, wakati naonyeshwa jengo na nilipoliangalia namna lilivyojengwa kuta zake na nondo zilizotumika bila shaka halikuwa na usimamizi mzuri,” Mhe. Rais Dkt. Samia alisisitiza.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameainisha kuwa, ni dhahiri fedha kidogo ndio iliyotumika kujenga jengo hilo kubwa la ghorofa nne bila kujali madhara yatakayotokea kutokana na jengo hilo kutokuwa imara.

“Wakati nikiwa nje ya nchi nilimuelekeza Waziri Mkuu kuunda timu ya uchunguzi na ameniarifu kuwa tayari imeundwa timu hiyo ya watu 20 ambayo inasubiri maelekezo rasmi ya Serikali ianze uchunguzi wa magorofa yaliyojengwa Karikakoo,” Mhe. Rais Dkt. Samia ameeleza.

Sanjari na hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, wakati zoezi la kusafisha eneo hilo likiendelea kuna ulazima kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuendelea kufukua kifusi ili kama kuna miili iliyosalia chini itolewe na ipate heshima ya kusitiriwa.

Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru wananchi wote waliofika katika eneo la maafa na kujielekeza katika kuwaokoa wahanga badala ya kutaka kuiba ili kujinufaisha na mali zilizopo katika jengo hilo.

Pia, Mhe. Rais ameelekeza, mali zote zilizopo katika jengo hilo ziende kuhifadhiwz mahali mpaka zoezi la uokozi na usafishaji wa eneo hilo ukamilike, ndio wafanyabiashara waende mahali hapo kutambua mali zao na kuzichukua na hatimaye kuendelea na shughuli za kujiingizia kipato.

Mhe. Rais Dkt. Samia ametembelea jengo la ghorofa nne lilioanguka kariakoo jijini Dar es Salaam, mara baada ya kurejea nchini akitokea Brasil alipoenda kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 kwa mwaliko wa Rais wa Brasil Mhe. Luiz Lula da Silva.








Post a Comment

0 Comments