Na mwandishi wetu
-Aagiza uhakiki wa madai ya Bi Martha ufanyike haraka kwa kuzingatia nyaraka stahiki.
-Aguswa na utafutaji wa Bi Martha amchangia milioni 2 ya kwake binafsi kama mtaji
-Atoa rai kwa wananchi kuwa na nyaraka stahiki pale wanapofanya kazi na Serikali
Na mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Machi 11,2025 amekutana na Bi Martha ambaye siku za hivi karibuni amesikika kupitia mitandao ya kijamii kuwa anaidai Hospitali ya Rufaa ya Amana zaidi ya shilingi milioni 3 kutokana na kufanya kazi ya kushona nguo za chumba cha upasuaji na kusambaza pazia, kazi ambayo ilifanyika 2017 na 2021.
RC Chalamila amepata wasaa wa kufanya mahojiano na Bi Martha mbele ya waandishi wa habari na watumishi wa Hospitali ya Amana juu ya mchakato mzima wa madai hayo na kumtaka Bi Martha kuleta nyaraka zitakazo muwezesha kulipwa kiasi hicho anachodai huku akimtaka mganga mfawidhi kuharakisha uhakiki wa nyaraka izo ili aweze kupatiwa haki yake anayostahili ambapo amesisitiza kuwa "Malipo ya Serikali hayawezi kufanyika bila kuwa na nyaraka stahiki, hivyo nyaraka zote zinzotakiwa ziwepo"
Aidha RC Chalamila amemchangia Bi Martha pesa tasilimu milioni 2 za kwake binafsi ili akaongeze mtaji katika biashara zake anazozifanya kwa kuwa ameonyesha kuwa mwanamke mtafutaji licha ya kuwa mjane.
Vilevile RC Chalamila ametoa rai kwa wananchi hasa wale wanaofanya kazi na taasisi mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanakuwa na nyaraka stahiki ili kuepuka kuchelewesha malipo yao.
Naye Bi Martha amekiri katika mkataba wake kuna vitu haviko sawa na ameridhika kwa ushauri aliopatiwa na Mkuu wa Mkoa pia amemshukuru kwa kumpatia shilingi milioni 2 kama mtaji wa biashara anayoifanya.
Kwa upande wa Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana Dkt Bryson Kiwelu amemshukukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwa karibu na Hospitali hiyo hali inayochangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma bora kwa jamii na amemuakikishia kutekeleza maagizo yake kwa wakati.
0 Comments