TAASISI YA APHI YAFANYA MATEMBEZI YA KIZALENDO KUTOKA KIGOMA MPAKA ZANZIBAR KIZIMKAZI

 


Na mwandishi wetu

TAASISI ya APHI Foundation imefanya matembezi ya hisani kutoka Kigoma Ujiji hadi Kizimkazi, Zanzibar kwa lengo la kuunga mkono mazuri yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hususan katika utunzaji wa mzaingira kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17, 2024 jijini Dar es Salaam kabla ya kuelekeza Kizimkazi, Zanzibar Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Philip Ally amesema kuwa huu ni msimu wa pili wa matembezi hayo yanayojulikana kama "Urithi Wetu Awamu ya Pili" huku kauli mbiu ikiwa ni "Mazingira yetu, urithi wetu".

Ally amesema kuwa matembezi hayo yanajumuisha jumla ya watu 39 ambapo wanawake ni 11 huku wanaume wakiwa ni 28 ambapo wanayatumia katika kuhamasisha mambo mawili ambayo ni utunzaji wa mazingira pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria (utalii).

"Haya ni matembezi ya hisani tumeanza matembezi yetu kuanzia Kigoma Ujiji na tunakwenda hadi Kizimkazi, Zanzibar. Katika matembezi haya tunahamasisha utunzaji wa mazingira na kutembelea maeneo ya kihistoria, lakini pia tumeandia hii historia," amesema Ally.

Kwamba katika utunzaji wa mazingira, maeneo waliyopita wamepanda miti ambapo hadi sasa kwa ushirikiano na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamepanda zaidi ya miti 20000 na sambamba na hilo wametumia fursa hiyo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwa upande wa maeneo ya kihistoria ni kwmaba, katika mikoa na Wilaya walizopita wametembelea meneo hayo na kuyaandika katika kitabu.

Ameeleza kuwa matembezi hayo ni ya kizalendo ambapo amebainisha kwamba mikoa waliyopita wameshuhudia ujenzi wa miradi mingi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia ikiwemo miundombinu ya Barabara, Hospitali na Vituo vya Afya, shule, maji na miradi mingine mingi.

Ally ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Samia kuendelea na kasi ya kulijenga Taifa kwa maslahi mapana ya Watanzania wote kwa kuendelea kuboresha miundombinu muhimu kwa maenedeleo ya kila Mtanzania.

Amewaka wazi kuwa matembezi hayo kwa Zanzibar yatapokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba hadi wanafika Dar es Salaam wametumia siku takribani 55 huku wakitembea zaidi ya kilometa 1250.

Kwa upande wake Chifu Mtwale ISembe wa Himaya ya Buha Kigoma Ujiji amemshukulu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Turiani jijini Dar es Salaam Mwalimu Janeth Mabusi kwa kuwapokea wanamatembezi hao na kuwahifadhi shuleni hapo kwa siku nne kabla ya leo kuelekea Zanzibar.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Turiani Mwalimu Mabusi amesema, kama shule wamejifunza kuwa matembezi ya hisani yanaweza kutumika katika kujenga uzalendo kwa nchi yetu pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika utunzaji wa mazingira hususan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Hata hivyo mmoja wa washiriki wa matembezi hayo Rehema Mangwa amebainisha changamoto walizokabiliana nazo njiani kuwa ni pamoja na kuvimba miguu, miguu kutoka malenge lenge na wakati mwingine kuchoka na kushindwa kutembea.




Post a Comment

0 Comments