Na Mwandishi Wetu, Manchester.
Kampeni ya kutangaza vivutio vya utalii kupitia Msafara wa mawakala 30 wa utalii katika bara la Ulaya ijulikanayo kama "My Tanzania Roadshow 2025' imehitimishwa tarehe 14 Machi 2025 katika Jijini Manchester nchini Uingereza.
Kampeni hiyo iliyojumuisha miji mitano iliyoko nchi nne za Ulaya ambayo ni Cologne (Ujerumani), Antwerp (Ubelgiji), Amsterdam (Uholanzi), London na Manchester (nchini Uingereza) imekuwa na mafanikio makubwa ambapo waandaaji wamefanikiwa kuvuka lengo la kuvutia Wakala au Wanunuzi wa Utalii kutoka Tanzania ambapo katika miji hiyo mitano zaidi ya Mawakala 240 wa nchi za Ulaya walihudhuria mikutano ya kibiashara baina yao na Wakala wa Utalii 30 kutoka Tanzania.
Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bw. Ernest Mwamwaja ameeleza kuwa katika kila mji mikutano hiyo imetoa fursa kwa Wakala wa Utalii wa Ulaya kupata taarifa za kutosha toka kwa taasisi za uhifadhi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo ni TTB, NCAA na TANAPA.
Ushiriki wa taasisi hizi umesaidia kutoa taarifa ya vivutio vilivyopo na kuelezea uboreshaji wa miundombinu ya utalii, mikakati ya Serikali ya utangazaji utalii, mwenendo wa utalii, juhudi za Serikali kuongeza mazao ya utalii, ubora wa huduma, na fursa za uwekezaji zilipo katika sekta ya utalii.
Mawakala wa Utalii kutoka Tanzania wameeleza kuridhishwa na kiwango cha ueledi katika maandalizi ya kampeni hiyo na ubora wa Wakala wanunuzi walioalikwa kukutana na Wakala toka Tanzania na kupanua soko la kupata wateja wa bara la ulaya.
Katika hatua nyingine, Bw. Mwamwaja amezishukuru ofisi za balozi za Tanzania katika nchi ya Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, na Uingereza kwa kuwa chachu ya mafanikio ya Kampeni hiyo na kuwataka Wakala walioko Tanzania kuendelea kuhudhuria midafara hiyo kila mwaka kuchangamkia fursa zinazoletwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kuitangaza Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Akihitimisha msafara huo Bw. Mwamwaja amemshukuru kipekee Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na juhudi zake binafsi za kutangaza Tanzania katika masoko ya kimkakati ya kimataifa.
Msafara kutangaza Utalii wa Tanzania My Roadshow 2025 umeratibiwa na Kampuni ya KiliFair ambapo ulianza tarehe 9- 14 Machi, 2025.
0 Comments