WAZIRI SILAA ATOA RAI KWA WADAU KUSHIRIKI KIKAMILIFU MCHAKATO WA SERA YA KAMPUNI CHANGA WAANZA

 


 

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Arusha.


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) amesema kuwa serikali tayari imeanza mchakato wa kutunga sera ya kampuni changa (startups) na imeanza kushirikisha wadau ili kutoa maoni yao kuhusu mahitaji ya startups na mambo wanayotaka kuona yakikamilika.

Waziri Silaa ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 13, 2025 jijini Arusha.

“Nia ya Mheshimiwa Rais ni kuona bunifu za startups zinasaidiwa na zinaweza kuvuka mipaka,” alisema Waziri Slaa.

Ameongeza kuwa, ni jukumu la Serikali kuhakikisha bunifu za kampuni changa (startups) zinaweza kufikia malengo.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amezindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024-2034 wenye nguzo sita, ambapo moja ya nguzo hizo ni kuhakikisha kuwa vijana hawa wanakuwa na maendeleo katika maeneo yao ya ubunifu”, amesisitiza Waziri Silaa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, aliwasihi vijana waliohudhuria mkutano huo kuomba nafasi za ufadhili wa masomo zinazotangazwa na Tume hiyo ili kuongeza ujuzi na kufanikisha malengo yao.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Umoja wa Kampuni Changa Tanzania (TSA), Bw. Zahoro Muhaji, alishukuru Wizara kwa kuandaa mkutano huo na kusema kuwa matarajio yao makubwa ni kuona vijana wakifanikiwa kupitia bunifu zao.

Dkt. Pamela Chogo, mdau wa startups, pia alishukuru Serikali kwa kuanza mchakato wa kuunda sera ya kampuni changa, akisema ni hatua jumuishi na wazi.








Post a Comment

0 Comments