CRDB,CARE INTERNATIONAL KUWAINUA WANAWAKE KUPITIA PROGRAMU YA IMBEJU

 


Benki ya CRDB imesaini makubaliano ya kushirikiana na Shirika la Care International kuwawezesha wanawake kupata mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa biashara, usimamizi wa fedha na mitaji, pamoja na kuwapatia mitaji wezeshi ya kujikwamua kiuchumi kupitia program ya IMBEJU.

Akizungumza kwenye hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema taasisi hiyo inafurahia kuingia mkataba wa ushirikiano na shirika la Care International kwani utakwenda kuwezesha programu ya IMBEJU kuwafikia wanawake wajasiriamali wengi zaidi nchini.


Tully amesema lengo ya programu ya IMBEJU ni kuongeza ujumuishi wa kiuchumi nchini, hivyo ushirikiano na Care International utakwenda kusaidia kufikia lengp hilo kwani shirika hilo limekuwa likijihusisha na uwezeshaji wa vikundi vya kiuchumi kote nchini kwa takribani miongo mitatu.

Tully amewakaribisha wabia wengine wa maendeleo nchini kushirikiana katika programu hiyo ya IMBEJU ili kuweza kuleta matokeo chanya zaidi na kuwezesha makundi ya vijana na wanawake.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Care International, Bi Prudence Masako amesema CRDB Bank Foundation ni mbia muhimu kwao kwani juhudi zao za kukabiliana na umasikini zitafanikiwa kutokana na uhakika wa fedha za uwezeshaji kupitia programu ya IMBEJU.

Mkurugenzi huyo amesema shirika la wa Care International lilianzishwa miaka 78 iliyopita lakini lina miaka 29 tangu liingie nchini na katika mkakati wake wa kusaidia jamii kupambana na umasikini linafanya kazi na vikundi zaidi ya 50 vyenye wanachama wasiopungua 600,000.

“Moja ya malengo makuu ya Care International ni kusaidia jitihada za kupunguza umasikini. Hivyo tuliposikia kuhusu programu ya IMBEJU tulifurahi kwani hii ni fursa ya kuwafikia watu wengi ambao wameachwa nyuma katika shughuli za kiuchumi. Vilevile tunaamini katika usawa, hakuna jamii imeendelea kama mwanamke hajaendelea,” amesema Prudence huku akiwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki programu ya IMBEJU.

Kunufaika na uwezeshaji kupitia programu ya IMBEJU wanawake wanatakiwa kuwa katika vikundi na kisha kuwasilishwa maombi kupitia tawi lolote la Benki ya CRDB nchini, au kupitia mfumo wa uwezeshaji wa vikundi wa Care International.


Vikundi vitatakiwa kusaini makubaliano ya kushiriki programu ya IMBEJU, na kisha kupatiwa mafunzo na Shirika la Care International au maafisa uweshaji wa CRDB Bank Foundation. Mitaji wezeshi inatolewa kwa mwanachama mmoja mmoja wa vikundi baada ya kuhitimu mafunzo.

Program ya IMBEJU ilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Machi 12 mwaka huu na kufungua dirisha la ufadhili kwa biashara changa za vijana na wanawake wajasiriamali. Zaidi ya Shilingi 5 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kupata mtaji wezeshi wa kuendesha biashara zao kupitia programu hiyo.


Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kulia)  akizungumza na waandishi wa habari wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa ushirikiano katika ya taasisi hizo kupitia programu ya IMBEJU unaolenga kuwawezeshawanawake wajasiriamali wengi zaidi kote nchini kupitia mafunzo na mitaji wezeshi iliyofanyika mwishoni mwa wiki makao makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.Wengine pichani ni na Mkurugenzi Mkazi wa Care International, Prudence Masako (katikati), na Mkurugenzi wa Miradi Care International, Haika Mtui.












Post a Comment

0 Comments