Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohammed Omar Mchengerwa ameshiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Jimbo lake Rufiji Mkoa Pwani
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mhe. Mohammed Mchengerwa leo Novemba 27, 2024, amekuwa miongoni mwa Watanzania walioitimia vyema haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa watakao waongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupiga kura katika kituo chake alichojiandikishia cha Umwe Mchikichini kilichopo Ikwiriri Jimboni kwake Rufiji Mkoa wa Pwani, Waziri Mchengerwa amesema taarifa alizonazo mpaka sasa uchaguzi unaendelea kwa hali ya amani na utulivu nchi nzima.
Katika maelekezo yake kwa wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi Waziri Mchengerwa amewataka wawe msaada kwa kuwasaidia kusoma orodha ya majina vizuri wapiga kura ili wote waliojiandikisha wapate fursa ya kupiga kura .
Alikadhalika amedokeza juu ya muda utakotumika kuhesabu kura hizo na kutoa matokeo ya jumla ya Nchi nzima akisema kanuni inatoa saa 72, lakini kwa mifumo ya kisasa ya mawasiliano waliyonayo OR - TAMISEMI kuna uwezekano mkubwa wa kumaliza zoezi hilo la kuhesabu kura mapema na hivyo kutoa taarifa ya jumla ya uchaguzi ili kujibu kiu ya watanzania.
Kuhusu suala la usalama Waziri Mchengerwa amewasisitiza wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa mikoa na wilaya kutofumbia macho viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani ili rai na mali zao Pamoja na miundombinu ya serikali ibaki salama.
0 Comments