DOYO ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS KUPITIA NLD

 


Taarifa

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo
Leo Tarehe 14 Machi, 2025, Mjini Morogoro

Ametangazo Nia ya Kugombea Nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo, Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), ametangaza rasmi nia ya kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Morogoro, Mheshimiwa Doyo alieleza kuwa, kwa heshima kubwa, anamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kumjalia kuwa na afya njema, pia amewashukuru Watanzania kwa muitika wao katika kukuza demokrasia nchini.

Mheshimiwa Doyo alisisitiza kuwa ni muhimu kukuza demokrasia ili kufikia malengo ya taifa letu. Aliendelea kusema kuwa, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia ambapo kila Mtanzania mwenye sifa anayo haki ya kuchagua au kuchaguliwa. Aliongeza kuwa, yeye mwenyewe ana sifa zote za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo umri usiopungua miaka 45, umri ambao tayari amevuka, na afya ya kuhimili majukumu ya urais anayo.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa uchaguzi huu, Mheshimiwa Doyo alisema kuwa uchaguzi huu ni wa sita tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, na hivyo ni uchaguzi muhimu sana kwa taifa letu. Alisisitiza kuwa, kama Mtanzania mwenye haki ya kikatiba, amejitathmini kifikra, kiuwezo, na kiuweledi, na kujiridhisha kuwa ana uwezo wa kumudu nafasi hiyo.

“Ndugu wa Tanzania, waandishi wa habari, kuja hapa kwangu si kwa mkupuo, bali ni kwa busara za wazee na familia yangu. Baada ya kuomba busara zao, waliniambia nenda, tuko na wewe. Si busara kuwataja hapa, lakini wanajua na wanasikia wakiwa pale walipo,” alisema Mheshimiwa Doyo.

Mheshimiwa Doyo aliendelea kusema kuwa bado kuna masuala mengi muhimu ambayo hayajapata kipaumbele kikubwa katika taifa letu, na hivyo ameamua kugombea nafasi hii ili kutoa mchango wake katika kushughulikia masuala hayo muhimu, kama vile:

1. Ajira

2. Elimu

3. Kilimo na Ufugaji

4. Rasilimali za Maji

5. Kuziba Mianya ya Ukwepaji wa Kodi na Kupambana na Rushwa

6. Kujenga Taifa la Walipa Kodi

7. Kuongeza Jitihada kwa Watoto wa Kike katika Elimu na Teknolojia

8. Kuimarisha Muungano wetu

9. Kuimarisha Sekta Binafsi ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kiserikali na kijamii

10. Kuweka nguvu katika Sekta ya Madini

“Kwa hiyo, nimeona ni muhimu kutoa mchango wangu katika taifa letu ili kuleta faraja kwa Watanzania. Hivyo, leo hapa mbele yenu, mimi Doyo Hassan Doyo, mwanachama wa Chama cha National League for Democracy (NLD), natangaza nia ya kugombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chetu cha NLD. Dhamira yangu ni kwenda kubeba dhana ya Uzalendo, haki, na maendeleo kwa vitendo ili tuwakomboe Watanzania,” alisisitiza Mheshimiwa Doyo.

NLD: Ukombozi wa Umma.
NLD: Mtetezi wa Umma.
NLD: Moto Moto Motooo!

Post a Comment

0 Comments