Na mwandishi wetu
Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA Musa Kuji amewataka Maafisa na Askari wa Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, bidii, nidhamu pamoja na ushirikiano ili kutimiza adhima na malengo ya kuimarisha shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo.
Kamishna Kuji aliyasema hayo jana Machi 15, 2025 alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli mbalimba na kufanya kikao na Maafisa na Askari hao katika ofisi za Makao Makuu ya hifadhi hiyo yaliyopo eneo la Kageye ndani ya Hifadhi hiyo iliyopo katika Mkoa wa Geita.
“Ninawapongeza sana Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo kwa kuchapa kazi na niendelee kuwasisitiza tuongeze bidii katika utendaji wa kazi na pia tuendelee kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na ushirikiano ili kuimarisha ulinzi wa maliasili za Taifa” alisema Kamishna Kuji
Akizungumza katika kikao hicho Kamishna Kuji alieleza dhamira ya Shirika ni kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi.
“Shirika letu litahakikisha linaendelea kuimarisha maslahi ya watumishi ikiwemo kuzingatia haki ya kujiendeleza kielimu, kutoa matibabu stahiki kwa mtumishi na wategemezi wake, haki ya watumishi kupandishwa vyeo pale vigezo vyote vinapokuwa vimezingatiwa na haki ya mtumishi kusikilizwa na kuthaminiwa” aliongeza Kamishna kuji.
0 Comments