Na mwandishi wetu
*• Ni pamoja na ujenzi holela wa majengo zikiwemo nyumba*
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, inatekeleza ahadi yake ya kuhakikisha ujenzi bora wa nyumba na miundombinu mingine, kwa kuwezesha utengenezwaji wa kanuni ya majengo (Building Code) itakayotumika kwenye ujenzi wa majengo mbalimbali nchini.
Utekelezaji huo unafanywa na Wizara ya Ujenzi kupitia Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), lenye jukumu la kuratibu na kuandaa miongozo mbalimbali inayotumika katika sekta ya ujenzi, ikiwemo Kanuni hiyo ya Ujenzi wa Majengo, kwa kushirikisha wadau wa ujenzi wakiwemo wataalamu kutoka taasisi za umma na binafsi.
Akizungumza katika kikao kazi cha kuandaa rasimu ya kanuni hiyo mjini Morogoro, Mbunifu Majengo kutoka katika Chama Cha Wabunifu Majengo nchini (AAT), T’chawi Mike amesema kukamilika kwa uandaaji wa kanuni hiyo na kutumika kutapunguza kero na athari mbaya mbalimbali zinazosababishwa na ujenzi usiozingatia kanuni.
Ametaja baadhi ya athari mbaya za ujenzi wa majengo usiozingatia kanuni za ujenzi kuwa ni pamoja na uwepo wa majengo yanayo karibisha majanga, ikiwemo kubomoka na, au kuanguka, majengo kutokidhi viwango vya ujenzi vinavyoruhusu uokoaji pindi hatari zinapotokea na athari mbaya nyinginezo.
Mhandishi Innocent Johnbosco wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) amesema, : ”Uandaaji wa rasimu ya kanuni hizi za ujenzi wa majengo umezingatia viwango vinavyotakiwa kitaifa na kimataifa, hivyo kutegemewa kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ndogo ya ujenzi wa majengo nchini.”
Aidha, Johnbosco, kama alivyoeleza Mhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Daudi Augustino, ameshauri elimu ya kutosha itolewe kwa watumiaji wa kanuni hiyo kabla ya kuanza kuitumia, ili kuepuka matumizi yasiyofaa yanayoweza kusababisha kuendelea kuwepo kwa changamoto za ujenzi wa majengo usio faa na kero nyingine zinazoepukika.
Sambamba na Dkt. Augustino anayetaka wigo wa ushirikishwaji upanuliwe zaidi katika uandaaji wa miongozo ya ujenzi na utoaji elimu kwa taasisi za elimu zinazozalisha wataalamu wa ujenzi, Mbunifu Majengo kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (FRF) Joseph Ngido amesema wako tayari kushiriki kuhakikisha matumizi sahihi ya kanuni hiyo.
Naye Mhandisi kutoka NCC, Magdalena Hyera amesema uratibu huu unaofanywa na Baraza la Taifa la Ujenzi ni utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.
0 Comments