Na Happiness Shayo-Iringa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezindua rasmi Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Misitu(National Forest Advisory Commitee- NAFAC) itakayojikita katika kutoa ushauri kwenye baadhi ya masuala yanayohusu Sekta ya Misitu hususan katika kukabiliana na changamoto za uvamizi kwenye maeneo ya misitu.
Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 10,2025 katika ukumbi wa hoteli ya Sunset, Mkoani Iringa.
“Kazi za Kamati kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ni kumshauri Waziri juu ya mambo yote yanayohusiana na ukodishwaji wa misitu, kutangazwa kwa hifadhi za misitu, usimamizi wa misitu ya hifadhi, mapitio ya sera ya misitu na mambo ambayo Waziri atahitaji ufafanuzi wake” amesema Mhe. Chana.
Amesisitiza kuwa Kamati hiyo imeundwa kutokana na umuhimu wa misitu nchini kwa kuwa moja ya nguzo muhimu za maendeleo ya uchumi kutokana na mchango wake kwenye Pato la Taifa.
“Rasilimali za misitu inakadiriwa kuchangia asilimia 3.5 kwenye pato la Taifa (GDP) na asilimia 10 ya biashara ya nje. Vilevile, Sekta ya Misitu inachangia kwa takribani asilimia tatu ya ajira rasmi nchini na ajira isiyo rasmi inafikia watu milioni tatu. Aidha, misitu inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Taifa kwa kutoa zaidi ya asilimia 75 ya vifaa vya kujengea”amesema Mhe. Chana.
Kwa upande wa huduma, Mhe. Chana amefafanua kuwa misitu ni muhimu katika kurekebisha mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi baioanuwai, miti dawa, kivuli na makazi ya wanyama na vyanzo vya maji kwa matumizi mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Mhe. Chana amesema Sekta ya misitu inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uvunaji haramu na uharibifu wa misitu iliyohifadhiwa, ubadilishwaji wa maeneo ya misitu kwa ajili ya matumizi mengine ya ardhi mfano makazi na kilimo cha kuhamahama, mioto kichaa, uwepo wa magonjwa na mimea vamizi, utamaduni uliojengeka wa kutumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia, utumiaji hafifu wa teknolojia na ubunifu kwenye uhifadhi, uhaba wa wataalam wa misitu, huduma hafifu za ugani wa misitu na upotevu wa misitu unaokadiriwa kuwa hekta 462,000 kwa mwaka.
Amesema uharibifu huo unahatarisha utulivu wa hali ya hewa, hasa upatikanaji wa mvua kwa wakati na kuvuruga misimu ya kilimo na shughuli nyingine za kibinadamu.
Hivyo kutokana na changamoto na mwenendo wa usimamizi misitu nchini, masuala mbalimbali yanahitaji ushauri wa NAFAC ikiwemo changamoto zinazohusu uvamizi wa hifadhi za misitu, namna ya utekelezaji wa mkakati wa kuendeleza misitu nchini na namna ya kushiriki fursa mpya zinazojitokeza mfano kushiriki kwenye biashara ya kaboni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Jumanne Maghembe (Waziri wa Maliasili na Utalii Mstaafu) ameshukuru kwa uteuzi wa nafasi hiyo na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yalitolewa kwa kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu wa misitu.
“Asante kwa maelekezo na vitendea kazi na ninasema kwamba tuko tayari kuifanya hii kazi hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan iko katika mageuzi ya kutumia nishati safi na kuachana na matumizi ya mkaa unaotokana na misitu” amesema Prof. Maghembe.
Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bernard Marcelline ameipongeza kamati hiyo kwa kuteuliwa katika kuendeleza uhifadhi wa misitu nchini.
“Ninyi ni timu makini katika uhifadhi na kuendeleza rasilimali za misitu, rasilimali uchumi na biashara” amesema Bw. Marcelline.
Hafla hiyo kuhudhuriwa na baadhi ya Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake, viongozi wa dini, pamoja na wanufaika wa rasilimali za misitu kutoka Mkoa wa Iringa.
0 Comments