SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA KAMPUNI YA BARRICK

 





*Kahama*


Imeelezwa kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa  wa kikazi na Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick ili kuendeleza uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni hiyo  kwa kushirikiana na Kampuni tanzu ya Twiga inayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa asilimia 16.

Hayo yameelezwa leo Julai 7, 2025 na Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa wakati akipokea taarifa ya utendaji kazi ya  robo mwaka  kutoka  Kampuni ya Barrick yenye  ubia na kampuni tanzu ya Twiga.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, kupitia ushirikiano wa Kampuni hizo kumekuwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa kila mwaka kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendeshwa kwa ushirikiano na wananchi mbalimbali  wanaozunguka mgodi huo.

Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, Kampuni ya Barrick kwa kushirikiana na Kampuni tanzu ya Twiga zitaendelea kufanya tafiti zake katika leseni yake ili kugundua maeneo mapya yenye rasilimali madini, hivyo wananchi wa maeneo husika wana  kila sababu ya kufuata Sheria zilizopo pindi mwekezaji anapotaka kuwekeza katika maeneo mapya yaliyogunduliwa kupitia tafiti zinazofanyika.

Akielezea kuhusu umuhimu wa utafiti unaofanywa na Kampuni hizo Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa, leseni 48 zilitolewa kwa wachimbaji wadogo zitaendelea kufanyiwa utafiti na maeneo yatakayogundulika na uwepo madini  yatagaiwa kwa wachimbaji wadogo ili kuendeleza uchimbaji wenye tija  utakao jenga  mahusiano mema baina ya mgodi na jamii inayozunguka mgodi.

Awali , akisoma taarifa ya utendaji kazi , Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick Mark Bristow amesema kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya ununuzi wa bidhaa na huduma umeendelea kufanyika kutoka Kampuni za kitanzania, ambapo asilimia 95 ya wafanyakazi wake ni watanzania.

Akibainisha mchango wa Kampuni Barrick, Bristow amebainisha kuwa, mpaka sasa Kampuni hiyo imeingiza  dola bilioni 4.79 katika uchumi wa Tanzania , ikiwa pamoja na dola milioni 558 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.

Sambamba na hapo, Bristow ameongeza kuwa, Barrick na Twiga wanaendelea kujenga miradi ya kijamii kama Mpango wa Ushirikishaji Jamii inayozunguka mgodi  unavyoelekeza ambapo kiasi dola za marekani milioni 30 zinapangwa kwa ajili ya kupanua miundombinu ya shule mbalimbali nchini.

Akifafanua kwa waandishi wa habari kuhusu eneo la Buzwagi ,  Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kuwa, eneo la Buzwagi  kwasasa limekuwa  Ukanda Maalum wa Kiuchumi (EPZ) na tayari wawekezaji mbalimbali  wameonesha nia ya kuendeleza uwekezaji wa kiuchumi.

Aidha, Dkt. Mwanga ameongeza kuwa, chuo cha Barrick katika eneo hilo (EPZ)kinatarajia kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa mafomeni zaidi ya 2,800 kutoka maeneo mbalimbali ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

*#InvestInMineralSectorTz* *#MineralValueAddition*




Post a Comment

0 Comments