UDOM Yaonesha Ubunifu na Uwezo wa Kitaaluma Maonesho ya 49 ya Sabasaba

 


Na mwandishi wetu

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, kuanzia Julai 1, 2025.

Katika banda lake, UDOM imewasilisha mafanikio ya utafiti, uvumbuzi na miradi mbalimbali ya wanafunzi na wahadhiri wake, ikiwa ni pamoja na teknolojia bunifu, tafiti za kiafya, kilimo, na maendeleo ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Umma wa chuo hicho, Bi. Amina Richard, amesema ushiriki wa UDOM katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wa chuo hicho kuonesha mchango wake katika maendeleo ya Taifa kupitia elimu, utafiti na huduma kwa jamii.

“Tumekuja kuonesha dunia uwezo wa wanafunzi na watafiti wetu. Tunawahamasisha wananchi watembelee banda letu wajifunze mambo mbalimbali, kupata ushauri wa kitaalamu na kuona jinsi elimu ya juu inavyoweza kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi,” amesema Bi. Amina.

Baadhi ya vivutio katika banda la UDOM ni pamoja na roboti zilizobuniwa na wanafunzi wa uhandisi, mifumo ya kidigitali kwa sekta ya afya na elimu, na tafiti zinazohusu mabadiliko ya tabianchi na kilimo bora.

Wananchi waliotembelea banda hilo wameeleza kuvutiwa na ubunifu wa wanafunzi pamoja na mchango wa chuo hicho katika kusaidia maendeleo ya jamii kwa vitendo.

Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yamejumuisha washiriki zaidi ya 3,500 kutoka ndani na nje ya nchi, yakibeba kaulimbiu isemayo “Tanzania: Kitovu cha Biashara, Viwanda na Uwekezaji kwa Maendeleo Endelevu”.

Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa mshiriki wa kudumu katika maonesho haya tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007, kikilenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla






Post a Comment

0 Comments