Na mwandishi wetu
Chama cha ACT Wazalendo kinakusudia kuwa na Mpango wa Chama wa kuhamasisha uhifadhi na ulinzi wa Mazingira kwa viongozi, wanachama na jamii kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu katika siku ya kwanza ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa ACT Wazalendo leo tarehe 03 Mei 2023.
Chama cha ACT Wazalendo kilichopata usajili wa kudumu tarehe 05 Mei 2014, kitaadhimisha kutimiza miaka 9 kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na kichama kwa siku tatu kuanzia tarehe 3-5 Mei 2023 katika Mkoa wa Pwani.
Leo tarehe 03 Mei, wanachama na viongozi wa Chama hicho wakiongozwa na Katibu Mkuu Ado Shaibu wamepanda miti na kufanya usafi wa mazingira kwenye Zahanati ya Mwandege katika Jimbo la Mkuranga.
Akizungumza baada ya shughuli hiyo, Ndugu Ado amesema wameamua kuyatumia maadhimisho ya miaka tisa ya ACT Wazalendo kupanda miti ili kushiriki katika utunzaji wa mazingira katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
"Nchi yetu na dunia kwa ujumla inakabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi. Madhara yake yameonekana kwenye sekta mbalimbali hasa za kilimo, nishati, utalii na maji. Uzalishaji wa chakula na umeme unashuka kila mwaka kwa sababu ya uhaba wa mvua" alisema Ndugu Ado na kuongeza,
"Ukiacha rai mbalimbali tunazotoa kwa Serikali kama vile kununua chakula cha ziada ili kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula na kutafuta vyanzo mbadala vya nishati ili kukabiliana na mgao wa umeme ambayo ni madhara ya moja kwa moja ya mabadiliko ya tabia nchi tumeona pia tushughulike na kiini cha tatizo kwa kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa vitendo. Ofisi ya Katibu Mkuu kwa kushirikiana na Msemaji wa Kisekta wa Mazingira, itakuja na Mkakati maalum wa kuwahimiza viongozi wa ngazi zote, wanachama na wananchi kwa ujumla kupanda miti na kuyatunza mazingira".
Shughuli za maadhimisho ya miaka 9 ya ACT Wazalendo zitaendelea kesho tarehe 04 kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii katika Jimbo la Mkuranga ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Ndugu Dorothy Semu, Makamu Mwenyekiti wa Chama Bara. Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kuwa kuwa tarehe 05 Mei.
Janeth Rithe, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano kwa Umma, ACT Wazalendo.
0 Comments