DC KOMBA ATAKA MAONESHO YA BRELA NA WADAU WAKE YATUMIKE KUTATHMINI HUDUMA ZINAZOTOLEWA

 


Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hashim Komba( katikati) leo tarehe 24 Oktoba, 2023, akikata utepe ikiwa ni ishara ya kufungua rasmi Maonesho ya BRELA na wadau wake yanayofanyika katika viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam, huku baadhi ya viongozi wa BRELA wakiongozwa na   Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa (wa pili kutoka kushoto) wakishuhudia zoezi hilo.

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Wilaya ya  Ubungo, Hashim Komba ametaka maonesho ya  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na wadau wake yatumike kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa sambamba na kuwa na madawati yanayowakutanisha wadau ili kupunguza watu wa kati (Vishoka) ambao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara. 

DC Komba amebainisha hayo leo Oktoba 24, 2023 alipokuwa akifungua maonesho  ya  kwanza ya BRELA na wadau wake, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Amewataka wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) na wadau wake kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao  ili biashara zao ziweze kukua.

“Wito wangu kwenu BRELA na wadau wengine wa maonesho haya ni kwamba tuhakikishe hawa wajasiriamali mbalimbali wanakua, hivyo wasaidiwe  kwa kupatiwa elimu ili waweze kurasimisha biashara zao,” amesema Komba.

DC Komba ametumia fursa hiyo kuitaka BRELA kuimarisha mahusiano na mazuri na taasisi zingine za Serikali hususan Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Serikali za Mitaa ambazo ndizo zinazowakutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

“BRELA, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania(TBS) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) shirikianeni katika utoaji wa elimu ili kudhibiti na kupambana na Bidhaa bandia, kuthibitisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali  na kuhakikisha wanafanya sajili mbalimbali  na kupata leseni,” ameongeza Komba.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema BRELA itaendelea kuwahamasisha wadau wake kurasimisha biashara zao kupitia majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki  katika maonesho. 

Maonesho ya BRELA  na wadau wake ambayo yatahitimishwa na mkutano wa Wadau Oktoba 27, 2023 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Da es Salaam, kauli  mbiu  yake ni “Urasimishaji Bashara katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.”

Post a Comment

0 Comments