THAMANI WOMEN TANZANIA YAZINDUA KAMPENI YA KITAIFA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO, SIMBA SC, AZAM FC NA SINGIDA FOUNTAIN GATE KUSHIRIKI

 




Na mwanahabari wetu,

TAASISI ya Thamani Women Tanzania imezindua kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa jinsia zote mbili inayojulikana kama ‘Piga Mpira Sio Mwanamke’.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo uliozihusisha klabu za Simba SC, Azam FC na Singida Fountain Gate FC uliofanyika leo Oktoba 18, 2023 jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Michezo,Sanaa na Utamaduni Hamisi Mwinjuma ameesema kama mwanamme mwenye mke na watoto wa kike na kiume amefarijika kwa kampeni hiyo.

"Mara nyingi hivi vilabu huwa tunaviona uwanjani vikipambana kwa ajili ya ushindi wa ligi kadhaa. Kama si Ngao ya Jamii basi, NBC Premier League au hii league mpya inayoanza hivi ijumaa ya tarehe 20 African Football League na kadhalika,” amesema Mwinjuma na kuongeza,

"Michezo imekuwa na uwezo wa kuwaunganisha watu na jamii na ina nguvu na kubwa katika miktadha yote. Kuanzia kiwango cha taaluma ya juu kabisa mpaka chini,watu wenye vipato tofauti,matabaka na dini tofauti. Michezo ina njia ya kuunda hali ya jamii kwa wale waliounganishwa kwa shauku hiyo,”.

Ameongeza kwa kusema “Kwa mfano, ukifuatilia Soka la hapa Tanzania na hata ligi za nje, unaweza kuona jinsi mashabiki walivyo na uwezo wa kushikamana mara moja na shabiki ambaye wamekutana naye hivi karibuni wa timu moja,”.

Ameeleza kuwa mchezo wa mpira wa miguu umesaida  kuunganisha watu na jamii kupitia uundaji wa mashujaa na, kadiri shujaa anavyo-jihusisha zaidi na jamii, ndivyo muunganisho unavyokuwa thabiti.

Kwamba jambo hili linapelekea mpira kuwa zaidi ya mchezo bali zana muhimu ya kuvunja vizuizi vya kijamii na kitamaduni nje ya uwanja; wachezaji kutoka nyanja mbalimbali wana jukumu la kufanya kazi pamoja kufikia lengo moja ushindi dhidi ya timu pinzani.

“Leo tuna-shuhudia vilabu hivi vitatu vikiungana dhidi ya mpinzani mmoja ukatili,” amesema Naibu Waziri Mwinjuma.

Naibu Waziri Mwinjuma amesema takwimu za tafiti tofauti, zinaonyesha kwamba Kitaifa, asilimia 40 ya wanawake wote wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili, wakati asilimia 17 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na kati ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49, asilimia 44 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au wa kijinsia na wenza wa karibu.

Ameeleza kwa kipindi kirefu swala la kupinga ukatili limekuwa likiongelewa na wanawake, hivyo ni wakati muafaka wa vijana wa kiume,kina baba wa makamu tofauti kulijadili janga hili la kitaifa ili kurithisha watoto Taifa lenye utulivu, amani,upendo na maendeleo.

Kwamba Wanawake wana mchango mkubwa sanaa katika maendeleo ya Taifa la Tanzania na maendeleo ya wanaume kwa ujumla.




Ameipongeza Taasisi Thamani Women Tanzania kwa kutumia michezo kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Ametumia fursa hiyo kuitaka jamii kuunga mkono bidii za Serikali ya Awamu ya Sita na Taasisi ya Thamani Women Tanzania kumaliza janga hili.

Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Thamani Women Tanzania Nafue Nyange amesema Taasisi hiyo imejitwika katika kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa jinsia zote mbili pamoja na mageuzi ya sheria zinazo athiri wanawake na watoto.

“Sambamba na uzinduzi wa  taasisi tunazindua rasmi kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake hali kadhalika watoto, Mama akinyanyasika mtoto anadhoofika kama si afya ya mwili basi ya akili,” amesema Nyange.

Amesema asilimia 58 ya wanawake na asilimia 40 ya wanaume wanaamini kwamba mume ana haki ya kumpiga mke wake palipo hali fulani ambapo asilimia 54 pekee ya wanawake nchini Tanzania waliofanyiwa ukatili wa kimwili au kingono wanatafuta msaada kwenye vyombo vya usalama,au kwa viongozi wa familia.

Naye Mbunge Mstaafu wa Tabora Mjini Ismail Rage ameipongeza Taasisi hiyo kwa uzinduzi wa kampeni hiyo.

Rage amesema kwamba kumpiga Mwanamke ni ushamba ameshauri bango la kampeni hiyo kuwekwa katika viwanja vyote vya mpira ili kila mtu afikiwe.

Mkurugenzi wa Simba SC Imani Kajula amesema kuwa klabu hiyo pamoja na Wachezaji wake watahakikisha wanaiwasilisha vyema kwa wananchi.




Post a Comment

0 Comments