DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 423.54 ZA SKANKA, YANASA WATUHUMIWA WA KUTENGENEZA BISKUTI ZA BANGI

 


Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lymo akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama skanka katika operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Hayo yamesemwa leo Novemba 8, 2023 na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lymo akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

“Kilogramu 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es Salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa, kilogramu 265.64 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya Nyanda za Juu Kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es salaam,” ameesema Kamishna Jenerali Lymo.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Lymo ameesema Mamlaka hiyo imekamata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na skanka katika eneo la Kawe jijini Dar es salaam.

Kwamba katika tukio hilo, watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi.

Vilevile amebainisha kuwa Mamlaka imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambazia na kuuza skanka kwenye fukwe za Bahari ya Hindi, Kwamba kutokana na operesheni hizo, watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita (6) wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Kamishna Jenerali Lymo ameeleza kuwa Skanka (skunk) ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol-THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida.

“Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica. Kiwango cha sumu kilichopo kwenye skanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10. Hivyo, skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka,” ameongeza Kamishna Jenerali Lymo.

Amesema imebainika kuwa, watu wasiowaaminifu huchanganya skanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu, sharubati, tomato sauce pia kwenye sigara na shisha.

Kwamba lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto.

Hivyo amewataka Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kuwa makini na vyakula wanavyovitumia na kuacha kufuata mikumbo isiyofaa ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua hali ambayo inaweza kuwaingiza  kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kufanya operesheni dhidi ya wasafirishaji na wazalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya haziendelei kuwepo nchini.

Amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya bure ya 119 ambapo taarifa zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi.







Post a Comment

0 Comments