Na, Mwandishi wetu Geita
Wananchi wa mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja ,Halmashauri ya Mji wa Geita,wamedai kuathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Geita Kutokana na kuzingirwa na maji kwenye makazi yao na kusababisha baadhi ya nyumba kuanguka na kuharibu mashamba yao kutokana na maji kujaa.
Wakizungumza na waandishi wa Habari ambao wamefika na kujionea adha kubwa ambayo wananchi wanapambana nayo kutokana na kujaa kwa maji kwenye makazi yao na kwenye mashamba.
Hellena Paul Misoji na Mashauli John ni wakazi wa mtaa huo wamedai mvua hiyo imesababisha hasara kubwa kutokana na kuharibu baadhi ya thamani za ndani na wengine wameyakimbia makazi hayo na kujikuta wakilala nje.
“Tumekuwa waanga wa muda mrefu sasa pamoja na malalamiko yetu tumeshayafikisha GGM kuwaomba watusaidia kuondoa tuta kwenye eneo ambalo maji yalikuwa yanaelekea lakini suala hili limekuwa ni gumu na kupelekea maji yanakosa mwelekeo yanakuja kwetu na kuathiri makazi yetu pamoja na mashamba kama mnavyoona waandishi”Hellena Misoji Mwananchi wa Mtaa wa Samina.
Mbali na kuharibu Makazi na Mashamba Mvua hiyo imeharibu pia kiunganishi cha Daraja ambalo walikuwa wanatumia wananchi wa mtaa wa Ikumbayaga,Samina na Mpomvu.
“Sio makazi tu sisi Zahanati yetu ipo Samina ndipo tulikuwa tunaenda kupata huduma za afya kwa sasa tumeshindwa inapelekea kuzungukia mjini kabisa na ni umbali mrefu madhara ya maji yamesababisha pia na daraja letu kuharibika na sasa hakuna mawasiliano kati ya mitaa mitatu”Abelnego Daud,Mkazi wa mtaa wa Mpovu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo Joseph Kazungu amesema madai ya wananchi ni ya kweli na athari ni kubwa ambazo zimetokea na kwamba pamoja na kufanyika kwa tathimi lakini hadi sasa wananchi wameshindwa kulipwa na kuhamishwa kwenye maeneo hayo suala ambalo limekuwa ni kizungumkuti huku akiiomba Serikali ya Kata,Wilaya na Mkoa wa Geita kuona uwezekano wa kuwasaidia wananchi wa mtaa wa Samina kwani athari zilizopo ni kubwa.
0 Comments