Na mwandishi wetu
●Kiasi cha Shilingi Bilioni 10 zakopeshwa kwa wachimbaji wadogo kutoka CRDB
●Ni mkopo wa Mtaji,manunuzi ya mitambo na utoaji huduma migodini
●Waziri Mavunde aipongeza Benki ya CRDB kwa kuinua sekta ya madini
●Wachimbaji wampongeza Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa sekta ya madini
*KAHAMA- SHINYANGA*
Kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na *Mh Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan* kupitia Wizara ya Madini inaendelea kuziaminisha sekta za fedha kuwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini nchini wanayo fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuendesha shughuli zao katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 19, 2024 na Waziri wa Madini *Mhe. Anthony Mavunde* mkoani Shinyanga katika hafla fupi ya utoaji wa mfano wa hundi ya shilingi bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa Madini ikiwa ni mkopo kutoka benki ya CRDB.
Waziri Mavunde amesema kuwa mikopo iliyotolewa itasaidia kuikuza na kuiendeleza Sekta ya Madini na hivyo kupelekea kuongeza kwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye pato la Taifa na uchumi wa nchi.
Waziri Mavunde ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa mkopo wa Bilioni 10 kwa wachimbaji wadogo na watoa huduma na kutumia fursa hiyo kuzitaka benki nyingine pia kuiunga mkono sekta ya madini kupitia utoaji wa mikopo.
Awali, akiwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Kutoa Huduma za Kifedha kwa wachimbaji wadogo nchini , Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB,*Ndg. Boma Raballa* amesema, Benki ya CRDB itaendelea kutoa mikopo kwa wachimbaji nchi nzima lengo likiwa kuinua katika mitaji ya kuendesha shughuli za uzalishaji madini nchini.Mpaka sasa Benki ya CRDB imetoa mikopo ya kiasi cha shilingi bilioni 64 ambapo shilingi bilioni 19 sawa na asilimia 30 zimeelekezwa kwa wachimbaji wadogo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,*Mh.Anamringi Macha* amesema mkoa wa Shinyanga ni moja ya mikoa ya kimadini ambao unatambua mchango wa sekta ya madini ambapo katika mwaka wa 2023/2024 ulifikisha asilimia 85 ya ukusanyaji wa maduhuli hivyo upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo utachochea shughuli za uchimbaji wa madini ambao utasaidia kuongezeka kwa mapato ya serikali.
Naye,Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, *Mhe.Masache Kasaka* ameipongeza Wizara ya Madini na taasisi zake kwa juhudi mbalimbali inazofanya katika mageuzi makubwa ndani ya sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Kamati ikiwemo hilo la kusimamia upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo.
Akitoa salamu, Rais Wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (*FEMATA*) *Ndg. John Wambura Bina* amempongeza Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Madini ambao umeanza kuleta tija na kuaminika kwa wachimbaji wadogo kukopesheka kwakuwa sasa kuna mashine za uchorongaji zinazosaidia kupata taarifa za awali za uwepo wa madini na hivyo kuwatoa wachumbaji kwenye kuchimba kwa kubahatisha.
0 Comments