BILIONI 46.3 KUBORESHA MIUNDOMBINU MANISPAA YA KIGOMA- MHE. KATIMBA

 


Na mwandishi wetu

#Awataka Wananchi kuitunza miundombinu itakayojengwa


#Mbunge wa Kigoma apongeza kupata Mkandarasi Mzawa


Na. Catherine Sungura,Kigoma


Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC) Manispaa ya Kigoma itagharimu shilingi za Tanzania Bilioni 46.3.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki la Katonga yaliyopo katika Manispaa ya Kigoma.

Mhe. Katimba alisema kwamba miradi hiyo itajumuisha mradi wa ujenzi wa barabara zenye urefu Km. 9.51 na mitaro ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa Km. 5.4 ambazo ujenzi wake unaendelea.

Alisema mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu katika eneo la Mwanga na Soko la Samaki katika eneo la Katonga ambao utagharimu shilingi bilioni 16.5.

“Ni matarajio yetu sote kuwa miradi hii italeta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na wageni mbalimbali ambao watanufaika na huduma za mahitaji mbalimbali ya vyakula na mavazi pamoja na mazingira bora ya kibiashara”.

Aliongeza kusema kwamba miradi hiyo pia itaongeza thamani ya maeneo husika  na hivyo kusababisha ongezeko la mapato kwa Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Kigoma.

Hata hivyo Mhe. Katimba amewataka wananchi kuitunza miundombinu itakayojengwa kwa gharama kubwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, alielekeza Halmashauri zenye miradi hiyo kuhakikisha inajiendesha  na kuzalisha mapato kwenye Halmaahauri husika.

Naye, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Mhe. Kilumbe Shaban Ng’enda alisema jambo hilo walilisubiri kwa muda mrefu na sasa limekamilika kwani itasaidia kuleta maendeleo katika mji wao na kuifanya Kigoma mpya.

“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa jambo hili kubwa, barabara zetu zitapendeza na tunaiona Kigoma mpya”.

“Tumefurahi tumepata Mkandarasi Mzawa tunaamini atafanya kazi kwa uzalendo kwani wana Kigoma tupo tayari kufanya kazi naye na kupata riziki kupitia ujenzi wa masoko haya”Aliongeza Mhe. Ng’enda.





Post a Comment

0 Comments