📌 *Wajadili Mikakati ya kuendelea kusukuma Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini*
📌 *Mhandisi Mramba aeleza Tanzania inavyopiga hatua utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia*
*Na mwandishi wetu*
*Baku,Azerbaijan*
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba, Mshauri wa Rais wa Masuala ya Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii, Mhe Angellah Kairuki na wataalam wengine wamekutana na Viongozi wa Taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforAll) kujadili namna Tanzania inavyoimarisha mikakati na kutafuta mashirikiano kwenye kusukuma ajenda ya nishati safi ya Kupikia
Wamefanya mazungumzo hayo katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP29) ulioanza leo jijini Baku nchini Azerbaijan.
Akizungumza katika kikao hicho cha uwili (Bilateral meeting) Mhandisi Mramba amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka lengo la kufikia 80% ya watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 ambapo kwa sasa Serikali inatekeleza ajenda hiyo kwa kuongeza kasi ya kusambaza miradi ya umeme vijijini (rural electrification)na ipo kwenye mpango wa kuandaa programu ya ugawaji wa majiko ya umeme ili kuongeza matumizi ya umeme kama nishati safi ya kupikia.
‘Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hii katika kuendelea kutekeleza mradi wa nishati safi ya kupikia katika baadhi ya shule zilizofikiwa na umeme nchini pamoja na kuzisaidia kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo tunatumia njia hiyo pia kuendelea kuhamasisha wanafunzi kujua umuhimu wa nishati safi ya kupikia tangu wakiwa wadogo."’ Amesisitiza Mha Mramba
Kwa upande wake Mshauri wa Rais kwenye Nishati Safi ya kupikia na Maendeleo ya Jamii, Mhe Angellah Kairuki amesema kupitia taasisi ya SEforALL na mahusiano mazuri iliyonayo kwa wadau mbalimbali, Tanzania itaendelea kujifunza namna nchi nyingine zinavyotekeleza ajenda hii ili kuhakikisha inakuwa na manufaa kwa Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya SEforAll, Bi Damilola Ogunbiyi amesema taasisi yao ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza masuala ya nishati safi ya kupikia hasa matumizi ya umeme kwenye kupika kuanzia Taasisi na kaya zilizokwishafikiwa na huduma ya umeme.
‘‘Tunaandaa Jukwaa la Kimataifa la masuala ya matumizi endelevu ya nishati litakalofanyika Mwezi Machi 2025 nchini Barbados ambapo tumemualika Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aje kuhutubia kama kinara wa nishati safi ya kupikia na namna anavyotekeleza ajenda hii ili kutoa hamasa kwa viongozi wengine kuunga mkono jambo hili’’.
Katika hatua nyingine, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, pamoja na Umoja wa Afrika wanaandaa mkutano wa pembezoni (Side event) uliopewa jina la “Kushughulikia Changamoto za Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika: Wito kwa Viongozi wa Afrika,” ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 12 Novemba 2024 ambapo katika majadiliano hayo Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Mhe.Dkt Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipambanua kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika, ikisisitiza umuhimu wa mbinu jumuishi katika kutatua changamoto za nishati na mazingira.
Mwaka 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan alizindua Mpango wa Kuwasaidia Wanawake wa Afrika katika Matumizi ya Nishati safi ya Kupika (AWCCSP) katika Mkutano wa COP28 ambao ulilenga kuongeza uelewa, kuunda ushirikiano, na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha ili kuongeza uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Vilevile tarehe 8 Mei 2024 Mhe Rais Samia alizindua mkakati wa nishati safi ya kupikia nchini.
Katika Mkutano wa COP29, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Taasisi zake za TANESCO, REA na TPDC zitashiriki katika Siku ya Nishati (Energy Day) kwa kufanya mawasilisho mbalimbali ya miradi na programu za Nishati zitakazosaidia kupunguza athari za Mabadiliko ya Tabianchi. Lengo la Siku hiyo ni kuwashirikisha Wadau katika kutangaza fursa zilizopo, kupata uelewa na kuongeza ushirikiano katika eneo hilo la Mabadiliko ya Tabianchi.
0 Comments