📌 *TANESCO yaunganisha Kigoma na umeme wa Gridi kupitia Kituo cha Kidahwe*
📌 *Mha.Nyamo-Hanga asema Serikali kuokoa sh.bilioni 58 zilizokuwa zikitumika kwenye umeme wa mafuta*
📌 *Ataja miradi mingine ya kuimarisha umeme Kigoma*
Agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt,Doto Biteko la kulitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutekeleza kwa kasi miradi itakayounganisha Mkoa wa Kigoma na Gridi ya Taifa kabla ya 2025 limetekelezwa kwa mafanikio baada ya Mkoa wa Kigoma sasa kutumia umeme wa gridi kupitia kituo cha umeme cha Kidahwe.
Dkt.Biteko alitoa agizo hilo tarehe 19 Septemba 2024 mkoani Kigoma wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa uzalishaji umeme katika mto Malagarasi (49.5 MW), uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV132 kutoka Igamba hadi Kidahwe na Kituo cha kusambaza umeme msongo wa kV 400/220/132/33 cha Kidahwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mha. Gissima Nyamo-Hanga ameeleza kuwa, Serikali kupitia TANESCO imejenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma kwenye Kituo cha Kidahwe yenye urefu wa kilomita 280 ambayo imewezesha Mkoa wa Kigoma kuungwa kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa.
Amesema kuwa, hatua hiyo imefanya Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 58.4 ambazo awali zilikuwa zikitumika kwa mwaka kuzalisha umeme kwa mafuta ya dizeli mkoani humo.
Mha. Nyamo-Hanga ameeleza kuwa huduma ya umeme katika Mkoa wa Kigoma sasa itakuwa bora zaidi kwa sababu ya uwepo wa umeme wa gridi ya Taifa ambao unazidi kutoa uhakika wa kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazotegemea umeme.
"Mbali na Mradi huu wa Kituo cha Kidahwe ambao umeunganisha Kigoma na gridi, tutaendelea na ujenzi wa Kituo kingine kikubwa zaidi chenye uwezo wa MVA 240 katika eneo hilihili la Kidahwe kwa ajili ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme ukizingatia shughuli za kiuchumi katika Mkoa huu zinakua kwa haraka, sisi kama Shirika tuliona tuongeze mradi huu ambao unatarajiwa kukamilika Novemba, 2026.” Ameeleza Mha. Nyamo-Hanga
Ameongeza kuwa, matumizi ya umeme katika Mkoa wa Kigoma yanatarajiwa kupanda mpaka kufikia Megawati 22 kutoka Megawati 17.5 za sasa kwa sababu Kituo hiko cha Kidahwe kina uwezo wa Megawati 54 ambazo zinazidi mahitaji ya Mkoa huo.
Sambamba na hilo, amesema kuwa mbali na kuwepo kwa Mradi wa Kituo cha Kidahwe, upo mradi mwingine unatekelezwa kwa lengo la kuvipatia umeme vijiji 18 ambavyo vipo jirani na mradi huo wa Kidahwe ambapo wateja 5000 wataunganishiwa umeme na hivyo kupelekea ongezeko la wateja kutoka idadi ya wateja 111,000 ya sasa.
Mradi wa Kituo cha Kidahwe ni mojawapo ya miradi ya kimkakati iliyotekelezwa na TANESCO kwa lengo la kuhakikisha mikoa yote nchini inafikiwa na Gridi ya Umeme ya Taifa.
0 Comments