Ofisi ya Taifa ya Mashtaka iwe ni Ofisi ya mfano katika kusimamia haki– DPP

 



Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu amesema  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ina  dhamira ya dhati ya kuona kuwa inakuwa mfano katika kusimamia haki kwa kujenga imani kwa wananchi na jamii nzima kwa ujumla.

“Tujenge imani kwa jamii na kwa wananchi, jambo la mwananchi likiwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka haitaji kutoa chochote bali aamini kwamba haki itatendeka, jambo hili litafanikiwa kama ninyi mnaoamua kushtaki ama kutokushtaki mtatenda kwa haki na kutokukubali kutumika iwe kwa maslahi binafsi ama ya watu wengine”.

Mkurugenzi wa Mashtaka amebainisha hayo wakati akifungua Kikao kazi na Mafunzo ya Nadharia na Vitendo kwa Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya na Waendesha Mashtaka Viongozi yanayofanyika tarehe 17 hadi 21 Desemba, 2024 Mkoani Pwani.

Amesema, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepewa jukumu kubwa na nyeti linalogusa haki za watu kwa kuwa wao  wanahusika na kutoa maamuzi ya kushtaki na wakati mwingine maamuzi ya kutokushtaki na hayo yote yanagusa haki za watu, na kwasababu hiyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa weledi wa hali ya juu na kwa uaminifu.

“Niwapongeze kwa kuwa mnajitahidi kutekeleza majukumu haya kwa uaminifu. Pamoja na kutekeleza majukumu hayo zipo changamoto kidogo katika utendaji wetu wa kazi ambazo zinapelekea kutotimiza wajibu wetu kwa kiwango kinachotakiwa.” Amefafanua hayo Mkurugenzi Mwakitalu.

Aidha, Mkurugenzi wa Mashtaka ameeleza kuwa timu ya Menejimenti imeweka mikakati mingi itakayowezesha kutatua changamoto hizo. Moja ya mkakati iliyowekwa ni kujenga uwezo wa watumishi kupitia mafunzo ya muda mfupi, mafunzo ya vitendo na mafunzo ya muda mrefu ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu na kuweza kuwahudumia wananchi ambao wanaangukia kwenye eneo lao husika la kimashtaka.

Amesema, mojawapo ya mikakati inayotekelezwa ni pamoja na kuwapa mafunzo Wakuu wa Mashtaka Wilaya na Waendesha Mashataka Viongozi kwa kuwa ndio nguzo muhimu kwenye utekelezaji wa majukumu hayo.

“Waendesha Mashataka Viongozi na Wakuu wa Mashtaka wa Wilaya ndio nguzo yetu, tunawategemea kwa kiasi kikubwa sana katika kuwahudumia wananchi kwenye eneo la kimashtaka. Ikiwa kama Ofisi matumaini na matarajio yetu makubwa kabisa yapo kwenu, hivyo niwaombe mfahamu na mlitambue hilo.” Amebainisha hayo Mkurugenzi Mwakitalu

Sambamba na hilo Mkurugenzi wa Mashtaka amewataka washiriki hao kuhakikisha wanaweka taarifa sahihi kwenye mfumo kila siku.

“Tumetumia gharama kubwa kuuandaa mfumo huu na kuuweka kwenye mwonekano mzuri unaoeleweka kwa urahisi, ni kwasababu tunataka mfumo huu utusaidie kupata taarifa na takwimu mbalimbali zitakazo tusaidia katika kufanya maamuzi.”

Aidha, amewataka washiriki kuongeza ushirikiano na wadau wa Haki Jinai ili kupata matokeo chanya katika uendeshaji wa mashauri ya Jinai.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bi. Bibiana Kileo amesema mafunzo hayo ni ya kipekee na ya muhimu kwani yamelenga kusaidia kuwaongezea ujuzi katika utendaji wao kazi na kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kushtaki.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Simon Ntobbi amewataka washiriki hao kwenda kutoa elimu kwa watumishi ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo.

“Tunataka mashauri yaweze kushughulikiwa kwa wakati na ushindi wa kesi uongezeke kwa kufuata misingi ya haki.” Amesema Mkurugenzi Ntobbi.

Post a Comment

0 Comments