DC SIMA AFIKA TARAFA YA KATERERO KUKAGUA UJENZI WA SHULE MPYA YA KATERERO YENYE HADHI YA NYOTA 5.

 



Na mwandishi wetu

 _Rais Samia atoa Milioni 584 kuijenga ikiwa na ICT Room, maktaba, maabara 3 za kisasa. DC Sima asisitiza hatua za mwisho kukamilika haraka ili ipokee wanafunzi._

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima Jana Jumamosi Januari 11, 2025 akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama amefika kwenye Tarafa ya Katerero kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Katerero iliyopo Kata ya Katerero inayogharimu takribani Milioni 584.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajenga Shule hiyo ya Kisasa sana ikiwa na majengo 11 yenye maabara 3 za sayansi za Biolojia, Fizikia, Kemia, Maktaba (library), chumba cha TEHAMA (ICT Room) na madarasa ya kutosha.

 DC Sima akikagua ujenzi wa shule hiyo amesema kata ya Katerero ilikua haina shule ya Sekondari hivyo wanafunzi wa kata hiyo wanalazimika kusafiri hadi kata ya Kemondo kusoma shule ya Sekondari Bujunangoma, kero ambayo sasa imeondolewa na Serikali ya Rais Samia kwa ujenzi wa shule hiyo.

"Hii ni shule ya mfano kwasababu ni ya kisasa sana na ina maktaba, maabara 3 za kisasa, chumba cha TEHAMA (ICT ROOM). Niombe Mkurugenzi Mtendaji na wasimamizi wa huu mradi tumalize mambo madogo madogo yaliyobaki ili wanafunzi waanze. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuona wananchi wa kata hii ambao hawakua na Sekondari lakini leo imejengwa shule hii ya kisasa sana." Alisema DC Sima wakati wa majumuisho baada ya kukagua ujenzi mzima wa shule hiyo kuanzia ramani, mikataba ya ujenzi na majengo yote. 

DC Sima na ujumbe wake walipokelewa kwenye mradi huo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukoba Bi. Fatina Laay aliyeambatana na Wataalamu wake, Afisa Tarafa ya Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku, Diwani wa Kata hiyo Mhe. Nuru Kabendera, Mtendaji wa Kata Bi. Sophia Busunge na Viongozi wengine.







Post a Comment

0 Comments