SERIKALI ITAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA UHAMIAJI - DKT. BITEKO



*📌 Aweka jiwe la msingi jengo la Uhamiaji na Makaazi ya Askari*


*📌 Dkt. Biteko awapongeza uhamiaji kwa kutoa huduma nzuri*


*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imekusudia kuendelea kuboresha huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo huduma za uhamiaji nchini ili kuharakisha maendeleo ya watu.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Januari 11, 2025 baada  ya kuweka Jiwe la Msingi katika jengo la Uhamiaji lililopo katika Wilaya ya Micheweni, Pemba ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofikia kilele chake Januari 12, 2025.

Amesema Wazanzibari na Watanzania wana kila sababu ya kujivunia maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambapo miradi mbalimbali imetekelezwa ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

“Mtakubaliana na mimi kwamba Serikali zote mbili zinaendelea kufanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Maendeleo haya ni matunda ya viongozi na waasisi Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema ujenzi wa Afisi na Makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamihaji ni ushahidi kwamba Serikali imenuia kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa tija.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Khatib amemshukuru Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa ya maendeleo sambamba na kuimarisha demokrasia.

Amesema wakati Wazanzibari wakiendelea kujivunia faraja zinazotokana na Mapinduzi, ni muhimu wananchi  kujua na kufahamiana ili kulinda usalama wa nchi. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Hamza Hassan Juma amesema maboresho yanayoendelea Wilaya ya Micheweni yamewaondoa katika hali ya umasikini.

Amesema uboreshaji wa miundombinu ya barabara na maji utachochea upatikanaji wa ajira kwa wakazi na hivyo kukuza uchumi na maendeleo.

Ameitaka Idara ya Uhamiaji kwa siku zijazo, kutafuta viwanja vya makazi tofauti na viwanja vya Afisi ili kulinda faragha za watumishi wanapokuwa kwenye mazingira ya makazi.

Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dkt. Anna Makakala, amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha masilahi na mazingira ya kazi kwa Maafisa Uhamiaji katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali itahakikisha mazingira ya kazi na utumishi ndani ya uhamiaji ili waendelee kuboresha huduma kwa wateja. 













Post a Comment

0 Comments