Dkt. Nungu Awataka Wabunifu na Watafiti Kuchangamkia Fursa ya Mkopo Nafuu



 

Na mwandishi wetu

Dar es Salaam, Aprili 17, 2025 – Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, ametoa wito kwa wabunifu na watafiti nchini kuchangamkia kwa haraka fursa ya mikopo nafuu inayotolewa kupitia ushirikiano kati ya COSTECH na Benki ya CRDB, kwa lengo la kuwawezesha kubadilisha mawazo yao ya kibunifu kuwa biashara zenye tija.

Akizungumza katika hafla utiaji saini wa makubaliano ya utoaji mikopo nafuu kwa wabunifu kupitia benki ya CRDB iliyofanyika katika Ukumbi wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Dkt. Nungu amesema kuwa mpango huo ni hatua madhubuti ya Serikali kupitia COSTECH kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha vijana na wabunifu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kidijitali.

“Mikopo hii nafuu si ya kusubiri, ni ya kuchangamkia. COSTECH iko tayari kutoa msaada wa kitaalamu, mafunzo, na ushauri kwa kila mbunifu au mtafiti mwenye wazo lenye mchango wa moja kwa moja kwa maendeleo ya taifa. Tunahitaji kuona mawazo haya yakigeuka bidhaa, teknolojia na huduma sokoni,” alisema Dkt. Nungu.

Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo, kiasi cha Shilingi Bilioni 4.6 kimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, ambapo kati yake, Serikali imetoa dhamana ya Shilingi Bilioni 2.3 ili kurahisisha upatikanaji wa fedha hizo kutoka kwa CRDB.

Dkt. Nungu alieleza kuwa mchakato wa kuomba mkopo umewekewa mfumo wa kidijitali ili kuhakikisha uwazi na usawa, na kwamba tayari zaidi ya wabunifu 400 wamefikiwa na programu mbalimbali za COSTECH zinazolenga kuwaandaa kwa fursa kama hizi.

“Tunataka kuona ujasiri wa wabunifu wetu katika kutumia fursa hii. Serikali imefanya kazi yake, sasa ni zamu yenu kuonesha dhamira, kuchukua hatua, na kuendeleza mapinduzi ya sayansi, teknolojia na ubunifu,” aliongeza. #wizarayaelimutanzania #ikulumawasiliano #crdbfoundation #Funguo_Tz #wfp

Post a Comment

0 Comments