Jopo la majaji katika Mahakama ya kikatiba limepiga kura kwa kauli moja kuunga mkono kushtakiwa kwa Yoon Suk Yeol.
Hii ina maana kwamba anaondolewa mara moja kwenye nafasi yake ya urais. Nchi hiyo sasa ina siku 60 kufanya uchaguzi wa haraka kujaza nafasi yake.
Akitoa hukumu yake jaji wa mahakama ya kikatiba nchini humo alisema hatua ya Yoon kutekeleza agizo la kijeshi ‘iliharibu haki za kimsingi za kisiasa za raia".
Jaji Moon aliongezea kuwa hatua hiyo "ilikiuka kanuni za utawala wa sheria na demokrasia".
Hatua ya Yoon ya kuwatuma wanajeshi kutekeleza sheria za kijeshi "inakiuka uhalali wa Bunge", Jaji Moon alisema, akimaanisha bunge la Korea Kusini.
“Hakutekeleza wajibu wake na alikwenda kinyume na raia ambao alipaswa kuwalinda,” alisema.
Mahakama pia iligundua kuwa hatua yake ya kutumia nguvu haikuhalalishwa, jaji alisema.
"Hakukuwa na hali ya dharura ya kitaifa," alisema Jaji Moon Hyung-bae, ambaye ni kaimu rais wa mahakama ya kikatiba.
"Ilikuwa hali ambayo ingeweza kutatuliwa kwa njia nyingine zaidi ya kutumwa kwa jeshi," alisema.
Rais Yoon hakufuata utaratibu alipotekeleza sheria ya kijeshi, jaji huyo aliongezea. Jaji sasa anapitia hoja za pande zote mbili - wale wanaounga mkono na wale wanaopinga mashtaka.
Mjadala ulikuwa juu ya iwapo tamko la Yoon la sheria ya kijeshi lilikuwa kinyume na katiba.
Hitimisho la hukumu hiyo linatarajiwa kutolewa hivi karibuni.
0 Comments