Na Mwandishi Wetu, Chalinze
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na halmashauri za Mkoa wa Pwani wametakiwa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni ya upandaji miti ili kufikia lengo la kupanda miti 13.5 milioni kwa mwaka.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani katika uzinduzi wa Siku ya Upandaji Miti uliofanyika katika Shule ya Msingi Chalinze Mzee, ambapo jumla ya miti 560 ilipandwa
Ndemanga alisema kila halmashauri inapaswa kupanda miti takribani milioni 1.5 kwa mwaka, na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili kudhibiti upotevu wa rasilimali.
“Uwiano kati ya miche tunayopanda na ile inayokomaa bado hautoshelezi. Hatuwezi kuendelea kutumia rasilimali nyingi kupanda miti ambayo haifuatiliwi wala kutunzwa. Ni lazima tuhakikishe miti tunayopanda inakuwa,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, Mathew Ntilicha, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, alisema upandaji miti ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa misitu kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Alibainisha kuwa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti hufanyika Machi 21 kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2025 yanaongozwa na kaulimbiu:
“Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali za Misitu kwa Kizazi cha Sasa na Kijacho.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Misitu wa Mkoa wa Pwani, Pierre Protas, alisema licha ya umuhimu mkubwa wa misitu kwa jamii, bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
“Changamoto tunazokabiliana nazo ni pamoja na uanzishaji wa makazi na mashamba katika maeneo ya misitu, utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama vyanzo vya nishati na kipato kwa jamii, pamoja na uhaba wa watumishi katika sekta ya maliasili,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi, Miriam Kihiyo, aliwataka walimu wakuu kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda na kutunza mti, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutunza mazingira. Alisema zaidi ya wanafunzi 61,000 wanatarajiwa kushiriki.
Aidha, aliomba TFS kusaidia upatikanaji wa dawa za kuzuia mchwa wanaoshambulia miti hiyo.
0 Comments