□ *Kufanya maandamano ya amani ya kumuunga mkono kila mkoa*
□ *Dkt. Kiruswa Abainisha mikakati ya kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo nchini*
*Awasihi kuweka maazimio hayo katika maandishi na kuwasilisha mbele ya Rais Samia*
📍 *Bariadi, Simiyu*
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, amesema kuwa wachimbaji wadogo wa madini nchini wameazimia kwa kauli moja kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuinua sekta ya wachimbaji wadogo.
Akizungumza katika Kongamano la Wachimbaji Madini wa Mkoa wa Songwe, leo Aprili 12, 2025, Bina amesema tangu Rais Samia aingie madarakani miaka minne iliyopita, sekta ya wachimbaji wadogo imepata mageuzi makubwa na ya kihistoria, na sasa wachimbaji hao wanaheshimiwa na kutambulika si tu ndani ya nchi bali hata katika mataifa mengine ya Afrika.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, dunia imeshuhudia mabadiliko makubwa. Wachimbaji wadogo sasa wanaheshimiwa na kuwa nchi pekee barani Afrika ambako kundi hilo linaheshimika, kusikilizwa na wamewekewa mazingira rafiki ya kufanya kazi zao.
“Tunamuunga mkono Mama Samia kwa vitendo. Haya mageuzi tunayoyaona leo ni matokeo ya uongozi wa kusikiliza, kushirikisha na kujali kila Mtanzania hata wale walioko kwenye sekta zisizo rasmi kama wachimbaji wadogo, leo tumeanza hapa Simiyu na tutafanya hivyo mikoa yote” amesema Bina.
Amezitaja sababu kuu zinazowafanya wachimbaji hao kumuunga mkono Rais Samia kuwa ni pamoja na Kuheshimika kwa Wachimbaji Wadogo; Upatikanaji wa Mikopo; Kuanzishwa kwa Masoko ya Madin; Upatikanaji wa Umeme Migodini; Kuongezeka kwa Ajira ambako Sekta ya uchimbaji mdogo imeendelea kutoa ajira kwa maelfu ya vijana na wakazi wa maeneo ya migodi, hivyo kusaidia katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuwainua wachimbaji wadogo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wachimbaji wakubwa na kutajirika kupitia shughuli hizi za uchimbaji madini. Tuna imani kuwa sekta ya wachimbaji wadogo itazidi kuwa injini muhimu ya uchumi wetu, na dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha hakuna mdau anayeachwa nyuma,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Pamoja na kupongeza uongozi wa FEMATA kwa hatua hiyo, Dkt. Kiruswa amewataka kuweka maazimio hayo katika maandishi ili wawasilishe kwa Mhe. Rais Dkt. Samia pindi watakapopata nafasi.
Dkt. Kiruswa amesema mikakati inajumuisha: kutenga maeneo ya uchimbaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo; Kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kupata teknolojia rafiki na salama za uchimbaji zikiwemo mashine za uchorongaji kupitia STAMICO; Kuimarisha mifumo ya utoaji wa mikopo kupitia taasisi za kifedha zinazoshirikiana na serikali sambamba na Kuwajengea uwezo wachimbaji kwa mafunzo ya mara kwa mara juu ya uchimbaji bora na usimamizi wa rasilimali; Kuratibu na kutatua changamoto za kisheria.
Naye, Mkuu wa Mkoa Simiyu Kenani Kihongosi amesema kuwa hatua ya FEMATA kuanza maandamano yao mkoani humo ni ishara ya kufunguka katika sekta ya madini sambamba na uwepo wa wachimbaji wadogo wengi ambao ni wanufaika wa mikakati madhubuti inayotekelezwa na Serikali kuhakikisha sekta inakuwa endelevu na kuchimba madini kwa tija na ufanisi.
0 Comments