KUTOKA KWA WAGOMBEA NA WATIANIA WA UBUNGE 55 WA CHAMA
CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) WA 2020 NA 2025,
WANAOWAKILISHA ZAIDI YA WATIANIA ZAIDI YA 200, WAKIWEMO
VIONGOZI WA JUU WA CHAMA
Tarehe 3/4/2025
KATIBU MKUU
CHADEMA – TAIFA
S.L.P 31191
Dar-es-Salaam
WARAKA MAALUM:
“USHAURI KWA CHAMA”
Husika na kichwa cha Waraka hapo juu.
Pia rejea wito uliotolewa na Ofisi yako kwa tuliokuwa wagombea ubunge wa CHADEMA 2020 na watia nia wa ubunge 2025, ukitutaka kushiriki kikao maalum pamoja na viongozi wakuu wa 6Chama, kilichopangwa kufanyika tarehe 3 April, 2025, kujadili hali ya kisiasa na mwenendo wa Chama katika kudai chaguzi huru na zenye kuaminika (No Reforms, No Elections)
I. MADHUMUNI YA WARAKA HUU
Pamoja na kupokea wito wa kushiriki mkutano huo maalum, sisi -wagombea ubunge wa 2020 na watiania wa ubunge wa 2025 – tumeona kuna viashiria vya kutopewa au kutopata nafasi yakutosha kusikilizwa katika mkutano huo maalum, na kwa hiyo, tumeamua kukuandikia Waraka huu, kwasababu zifuatazo:
1. Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mhe Tundu Lissu, akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Iringa ametamka wazi kuwa, “wote wanaoona, “No Reforms, No Elections” haiwezekani ni wana-CCM pamoja na vibaraka wao”. Kauli hii ya Mwenyekiti tayari imezuia uhuru wetu wa kutoa maoni au ushauri mbadala dhidi ya “No Reforms, No Elections”, kwani, kwa mujibu wa Mwenyekiti wetu, watu wa namna hiyo ni wana-CCM au vibaraka wao.
2. Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa Kamati ya Chama ya kuchangisha fedha kwaajili ya “No Reforms, No Elections”, Mhe Godbless Lema, akihutubia mkutano jijini Arusha, amenukuliwa akisema kwamba “wote wanaotaka ubunge au udiwani bila reforms waondoke CHADEMA”. Kauli hii ya Mhe Lema ya kufukuza watu wenye maoni
mbadala ndani ya Chama, haijakanushwa na Chama, na inazidi kuondoa mantiki ya mkutano huo maalum wa kujadili mwenendo wa “No Reforms, No Elections”, kwani tayari washiriki tumewekewa mipaka na vitisho katika kujadili suala hilo.
3. Hivi karibuni, Mwanaharakati, Maria Sarungi, aliandika katika ukurasa wake wa “X”akikitaka Chama kiyaweke hadharani majina ya wote wanaotaka ubunge kwa udi na ubani bila reforms, na akatuhumu kuwa watu hao wanataka kufanya “blackmail” (kutishia) eti watahama chama. Pia, Maria Sarungi, bila kujali mamlaka ya Ofisi yako, ametaka ajulishwe ni nani amewaita watiania kwenye mkutano huo maalum maana uongozi mzima upo field. Na akataka Chama kisiwahusishe watiania (“do not engage them”), bali waachwe waende CCM. Kauli hizi za Maria Sarungi (ambaye si MwanaChadema), zinafanana na kauli za Mhe Lissu na Mhe Lema. Aidha, kauli hizi zinaingilia mamlaka ya ndani ya Chama, na Ofisi yako imezinyamazia kimya, huku kukiwa na taarifa kuwa Mwanaharakati huyo ana mgongano wa kimaslahi wa kutaka Chama kisishiriki uchaguzi wa mwaka huu kwa maslahi yake binafsi. Kauli za Maria ambaye ni swahiba wa karibu wa baadhi ya viongozi wetu wakuu zinazidi kuongeza vitisho na kufinya uhuru wa maoni kuelekea katika kikao hicho maalum.
Kwa msingi huo, tunawasilisha mchango wetu wa mawazo kwa njia ya maandishi kama ifuatavyo:
II. TUNAUNGA MKONO MADAI YA MABADILIKO (REFORMS)
Tunaunga mkono na tupo tayari kuongeza nguvu zaidi katika jitihada zote za Chama za kudai mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi (reforms) ili kuwa na chaguzi huru na zinazoaminika.
III. MAONI MBADALA DHIDI YA MPANGO WA KUZUIA UCHAGUZI
Tunasita kuamini katika mpango wa Chama wa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2025 (iwapo mabadiliko hayatopatikana), tukiwa na sababu kuu zifuatazo:
1. Tunaona kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya uchaguzi. Kujaribu kuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi itakuwa ni sawa na kufanya jinai. Uwezekano pekee wa kuzuia uchaguzi ni kushiriki uchaguzi wenyewe kwa kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi. Ni rahisi kwa wagombea kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahsusi vya uchaguzi, katika kata au majimbo yanayoelekea kufanyiwa hujuma kuliko kujaribu kuzuia uchaguzi wote huku tukiwa nje kabisa ya uchaguzi wenyewe.
2. Dhana ya “No Reforms, No Elections”, ilianza kama kampeni mnamo mwezi Januari mwaka 2020 baada ya “retreat” ya Kamati Kuu iliyofanyika Makueni, nchini Kenya, na haikuwa na tafsiri ya kuzuia uchaguzi bali ilikuwa inalenga kuhamasisha uungwaji mkono wa kudai reforms.
3. Kwa muda mfupi uliosalia, hatuoni uwezekano wa kutekeleza kwa ufanisi mkakati wowote madhubuti wa kuzuia uchaguzi. Tayari, uchaguzi wenyewe umeshaanza kupitia zoezi la uandikishaji wapiga kura ambalo limeshafanyika kwenye mikoa mingi nchini na mchakato wa uchaguzi unaendelea kwa hatua ya mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
4. Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, ibara ya 4 inayohusu madhumuni ya Chama, dhumuni kuu la Chama ni kuongoza dola na kutekeleza madhumuni mahsusi ya kisiasa kama yalivyoainishwa katika kifungu cha 4.1, madhumuni ya kiuchumi yaliyopo kwenye kifungu 4.2 pamoja na madhumuni ya kijamii kama yalivyoainishwa katika kifungu 4.3.Kwa hiyo, kushiriki uchaguzi ili kuongoza dola ni sharti la kimsingi la kikatiba.
5. Ibara ya 5.2.2 ya Katiba ya Chama imetamka haki ya mwanachama wa CHADEMA kuwa ni pamoja na kuchaguliwa kuongoza na kuwakilisha Chama katika ngazi yoyote kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa ya sifa za uongozi. Mpango wa kuzuia uchaguzi unaweza kukosa uhalali wa kutosha kikatiba kwa kuathiri haki za wanachama wa CHADEMA wanaotaka kugombea.
6. Ukiondoa chama chetu, mpaka sasa hakuna chama kingine hata kimoja cha siasa kinachounga mkono mpango wa kuzuia uchaguzi ikiwa reforms hazitopatikana. Kinyume chake, kuna Chama kimoja tu cha upinzani ambacho kinapigania “reforms” lakini hukukikiendelea kujipanga kushiriki uchaguzi. Vyama vingine hususani vile vyenye kawaida ya kutumika na CCM, vimeendelea kutangaza nia zao za kushiriki uchaguzi.
7. Viongozi wa dini na madhehebu yenye waumini wengi hapa nchini, tayari wamehimiza na wanaendelea kuelimisha na kuhamasisha waumini wao kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwaajili ya kushiriki uchaguzi. Hali hii inaashiria kuwa ni ama Chama chetu kimechelewa au tayari kimekwama kupata uungwaji mkono wa wadau muhimu katika mpango wa kuepuka uchaguzi usio na reforms.
8. Uchunguzi na uchambuzi wetu unaonesha kuwa wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai yetu ya “reforms”, lakini wanasita kuunga mkono mpango kamili wa Chama chetu wa kuzuia uchaguzi iwapo “reforms” hazitopatikana, kwani hali hiyo kwao inatafsiriwa kuwa ni karibu sawa na kufanya uasi au kuvunja katiba na sheria zilizopo licha ya ubaya wake. Kwa maneno mengine, msisitizo wa kuzuia uchaguzi unaathiri au kupunguza kasi ya uungwaji mkono katika madai ya msingi ya reforms.
9. Kushindwa kuzuia uchaguzi katika dakika za mwisho (ikiwa jitihada za kupata reforms zitakwama), kunamaanisha kuwa Chama hakitokuwa tena na muda wa kujiandaa nahivyo hakitoshiriki kabisa uchaguzi huo.
IV. ATHARI ZA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI
Mhe Katibu Mkuu, matokeo ya kushindwa kuzuia uchaguzi yatakuwa ni kutoshiriki uchaguzi. Katika moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari, Makamu Mwenyekiti wa Chama, Mhe John Heche, alithibitisha ukweli huu pale alipojibu swali la Chadema itafanyeje iwapo haitofanikiwa kuzuia uchaguzi. Mhe Heche, aliweka bayana kuwa “ikiwa hivyo basi Chama hakitoshiriki uchaguzi”. Ni maoni yetu kuwa Chama kitafikwa na athari zifuatazo iwapo hakitoshiriki uchaguzi:
1. Chama kinaweza kuondokewa au kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kuwania urais, ubunge, udiwani pamoja na nafasi za viti maalum vya ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini.
2. Chama kitapoteza mvuto kwa umma, kitadhalilishwa kwa propaganda na hata kudhohofika. Hadi sasa Chama kimekatika katika vipande viwili vinavyosigana kuhusu jambo hili. Ikitokea tukashindwa kushiriki uchaguzi, mkatiko huu utakuwa ni wa wazi na athari zake zitakuwa mbaya zaidi.
3. Chama kitapoteza kabisa ruzuku baada ya uchaguzi na hivyo kuathiri uhai na uendelevu wa shughuli za Chama.
4. Ari na hamasa ya wanachama kukichangia Chama itazidi kushuka kwani wananchi hawatoona faida ya kukichangia Chama kisichoshiriki uchaguzi.
5. Kutoshiriki kampeni na uchaguzi kutakipotezea Chama fursa ya kujijenga zaidi maana haitokuwa rahisi kwa watiania kuwekeza kwenye Chama ambacho hakiingii kwenye uchaguzi maana hawatopata fursa ya kugombea.
6. Kwa ujumla, kutoshiriki uchaguzi kutasababisha Chama kupoteza uhusika na umuhimu wake kwa umma (relevance), hali inayoweza kufuatiwa na kuporomoka kisiasa na hatimaye kudhohofika kabisa.
IV: USHAURI WETU: TUJIANDAE KWA UCHAGUZI
Kwa hiyo, kwa kuzingatia msingi wote huo, sisi tuliokuwa wagombea ubunge 2020 na watiania wa ubunge 2025, tunakishauri Chama chetu (CHADEMA) kwamba tuendelee na tuongeze kasi na nguvu ya kudai mabadiliko yatakayoleta chaguzi huru na zenye kuaminika (reforms), lakini bila kuchanganya madai hayo na ajenda ya kuzuia uchaguzi. Badala yake, Chama kiruhusu kuanza mara moja kwa maandalizi ya chini kwa chini ya kujipanga kwaajili ya kushiriki uchaguzi hata kama reforms zitakuwa zimekawia kupatikana.
Tunatoa ushauri huu tukiwa ni wana-Chadema makini, wenye mapenzi mema na uaminifu wa hali ya juu kwa Chama chetu, huku tukisukumwa na maslahi mapana na endelevu ya Chama na nchi yetu. Katika ushauri wetu huu, tumetilia maanani masuala ya msingi yafuatayo:
1. Upo uwezekano wa kushinda uchaguzi wa 2025 na kutangazwa katikati ya vikwazo vingi vya kikatiba, kisheria na utamaduni mbaya wa CCM wa kubaka demokrasia. Pamoja na hujuma na uonevu wote tuliofanyiwa katika chaguzi zilizopita, bado yapo madhaifu ya ndani ya kirasilimali na kimkakati yanayoweza kuondolewa na hivyo kukifanya Chama kiingie katika uchaguzi huu kikiwa na nguvu mpya na mikakati madhubuti ya kukabiliana na hujuma za CCM na serikali yake kwa kiasi kikubwa. Zipo nchi nyingi duniani na ndani ya Bara la Afrika ambazo vyama vya upinzani viliweza kupambana na kushinda chaguzi katikati ya mazingira onevu na kandamizi ya katiba na sheria za uchaguzi. Wakati tukipigania reforms, tuchukue vile vile wajibu wa kuandaa mkakati kabambe wa kuikabili CCM katika mazingira magumu ikiwa reforms hazitopatikana kwa wakati.
2. Tukijipanga vizuri kimkakati, kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa kubwa na nzuri zaidi ya kuuzuia uchaguzi kirahisi kwenye vituo na maeneo mahsusi yanayoelekea kufanyiwa hujuma. Tunasisitiza kuwa ni ngumu na kwa kweli haiwezekani kuuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi.
3. Kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa ya ziada ya kuyatumia madhila ya uchaguzi katika kuwaunganisha, kuwachochea na kuwaongoza wananchi kuendeleza vuguvugu la kudai reforms kwa kishindo kikubwa zaidi.
4. Kushiriki uchaguzi kutasaidia kuimarisha na kuendeleza umoja na mshikamano wa Chama, wanachama na wananchi, kutahuisha uhai na kuendeleza nguvu, hamasa na harakati za Chama (mabadiliko ni mchakato)
5. Ikumbukwe kwamba, pamoja na mapungufu makubwa ya katiba na sheria za uchaguzi, bado si hujuma zote tunazofanyiwa katika chaguzi zimetamkwa au zimehalalishwa katika kisheria. Vitendo vya mawakala wetu kutoapishwa, mawakala wetu kuzuiwa kuingia vituoni, wagombea wetu kunyang’anywa fomu, wasimamizi kukimbia ofisi ili kukwepa kupokea fomu za wagombea wetu na kura feki kuingizwa vituoni, si matendo ambayo yamehalalishwa na katiba wala sheria bali ni uhuni tu unaofanywa na CCM na serikali yake na ambao upo kinyume pia na sheria zilizopo. Kwa hiyo, mbali na kupigania reforms kwaajili ya kuleta chaguzi huru na zenye kuaminika, kushiriki uchaguzi kutatupatia fursa ya kuja na mikakati madhubuti ya kukabiliana moja kwa moja na vitendo vya kihuni vilivyo kinyume kabisa na sheria zilizopo.
V. HITIMISHO
Mheshimiwa Katibu Mkuu, tunaomba uzingatie kuwa tumetoa maoni na ushauri wetu huo baada ya Ofisi yako kutualika kujadili ajenda ihusuyo hali ya kisiasa na mwenendo wa Chama katika kudai chaguzi huru na zenye kuaminika.
Kwa muhtasari, maoni na ushauri wetu, vimejikita katika kuunga mkono madai ya reforms lakini wakati huo huo tukikisihi Chama chetu kione haja ya kujiandaa na hatimaye kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 hata kama reforms hazitopatikana kwa wakati. Kwamba, kushiriki uchaguzi kutatuepusha na athari nyingi na za muda mrefu za kudorora kwa Chama, huku tukiwa pia na uwekezakano wa kushinda au kuzuia uchaguzi kwenye maeneo au mazingira mahsusi ya kiuchaguzi yatakayoelekea kufanyiwa uhuni au hujuma dhidi ya demokrasia.
Tunaomba Chama kiyazingatie, kiyape kipaumbele katika tathmini na tafakari zake na kiyafanyie kazi maoni na ushauri wetu huo kwa kina, kikiongozwa na fikra chanya, maslahi mapana na endelevu ya Chama, pamoja na nafsi zilizojaa upendo, umoja na mshikamano kwa wana-Chadema wote.
Tunapenda kusisitiza kuwa maoni na ushauri wetu huo si wa kupinga msimamo wa Chama, bali ni wa kupendekeza namna bora zaidi ya kuziendea reforms huku tukilinda ustawi endelevu wa Chama chenyewe chini ya imani kuwa “change is a process” (mabadiliko ni mchakato).
Tunapenda ieleweke kuwa iwapo Chama hakitakubaliana na maoni na ushauri wetu, basi tutaendelea kuheshimu msimamo na mwelekeo wa Chama kwa uaminifu na mapenzi yetu yote.
Pamoja na salaam za “Stronger Together”
Mungu ibariki Chadema, Mungu ibariki Tanzania.
Tunaomba kuwasilisha.
Ni sisi, Wagombea Ubunge wa 2020 na Watiania wa Ubunge, 55 (CHADEMA) wa 2025, tunaowakilisha zaidi ya watiania 200, kutoka majimbo mbalimbali ya Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar, wakiwemo viongozi wa juu wa Chama.
1. Mhe. John Mrema – Jimbo la Segerea
2. Mhe. Catherine Ruge – Jimbo la Serengeti
3. Mhe. Julius Mwita – Jimbo la Musoma Mjini
4. Mhe. Suzan Limbweni Kiwanga – Jimbo la Mlimba – Morogoro
5. Mhe. Grace Sindato Kiwelu – Jimbo la Vunjo - Kilimanjaro
6. Mhe. Daniel Naftari Ngogo – Jimbo la Sumbawanga Mjini – Rukwa
7. Mhe. Henry Kilewo – Jimbo la Kawe – Dar-es-Salaam
8. Mhe. Francis Kishabi – Jimbo la Kisesa – Shinyanga
9. Mhe. Gervas Mgonja – Jimbo la Same Magharibi – Kilimanjaro
10. Mhe. Edward Edmond Kinabo – Jimbo la Kibaha Vijijini – Pwani
11. Patrick John Assenga – Jimbo la Segerea – Dar-es-Salaam
12. Elia Evarist Gregory – Jimbo la Kigoma Kusini – Kigoma
13. Hadija Said Mwago – Jimbo la Temeke – Dar-es-Salaaam
14. Exaud Mamuya – Jimbo la Vunjo - Kilimanjaro
15. David Nuhu Chiduo – Jimbo la Kilosa - Morogoro
16. Glory Tausi Shayo – Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki - Morogoro
17. Benjamin Kambarage – Jimbo la Kinondoni – Dar-es-Salaam
18. Blackwell Kayuni – Jimbo la Ileje - Songwe
19. Bumija Moses Senkondo – Jimbo la Kibaha Vijijini - Pwani
20. Lembrus K. Mchome – Jimbo la Mwanga - Kilimanjaro
21. Michael Kilawila – Jimbo la Moshi Mjini – Kilimanjaro
22. Mhe. Shabani Matimbwa – Jimbo la Rufiji – Pwani
23. Mhe. Salma Shariff – Jimbo la Bagamoyo - Pwani
24. Mhe. Juma Magwede – Jimbo la Rufiji – Pwani
25. Mhe. Vitus Nkuna – Jimbo la Kyerwa – Kagera
26. Yosepher Ferdinand Komba - Jimbo la Muheza – Tanga
27. Mhe. Herman Cosmas Kiloloma – Jimbo la Mbagala – Dar-es-Salaam
28. Mhe. Richard Mbalase – Jimbo la Rungwe – Mbeya
29. Mhe. Emma Kimambo – Jimbo la Arusha Mjini – Arusha
30. Mhe. Ayubu Exaud – Jimbo la Arumeru Magharibi – Arusha
31. Mhe. Mathayo Torongey – Jimbo la Bagamoyo – Pwani
32. Mhe. Rashidi Kilumbi – Jimbo la Chalinze – Pwani
33. Mhe. Rachel Mkadala – Jimbo la Segerea – Dar-es-Salaam
34. Mhe. Lilian Kimei – Jimbo la Vunjo – Kilimanjaro
35. Mhe. Andrew Masenya – Jimbo la Ilemela – Mwanza
36. Mhe. Adv. John Mallya – Jimbo la Arusha Mjini – Arusha
37. Mhe. Peter Andrea Matyoko – Jimbo la Ilemela – Mwanza
38. Mhe. Emmanuel R. Mtobi – Jimbo la Shinyanga Mjini – Shinyanga
39. Mhe. Paul James Mayani – Jimbo la Kigoma Mjini – Kigoma
40. Mhe. Geofrey Benedicto Andrea – Jimbo la Kindondoni – Dar-es-Salaam
41. Mhe. Gerald Kazonda – Jimbo la Kwela – Rukwa
43. Mhe. Bruce Cuthbert – Jimbo la Iringa Mjini – Iringa
44. Mhe. Solomon Mnamunga – Jimbo la Korogwe Vijijini – Tanga
45. Mhe. Bosco Mfundo – Jimbo la Gairo – Morogoro
46. Joseph Wamajiwa Teute – Jimbo la Rorya - Mara
47. Mhe. Boniface Kimario – Jimbo la Rombo – Kilimanjaro
48. Upendo Ngonyani – Jimbo la Biharamulo – Kagera
49. Mhe. Lucy Magereli – Jimbo la Kigamboni - Pwani
50. Mhe. Paul Juma Kija – Jimbo la Kilindi – Tanga
51. Mhe. George E. Mwaipungu – Jimbo la Lupa
52. Mhe. Sulus John Matutu – Jimbo la Ilemela - Mwanza
53. Mhe. Hanifa Kassim Chiwili – Jimbo la Rufiji – Pwani
54. Mhe. Francis Msuka – Jimbo la Katavi – Katavi
55. Mhe. James Erick Kabepele – Jimbo la Igalula –
0 Comments