RAIS MWINYI:TUMUENZI HAYATI MSUYA KWA KUENDELEZA MAONO YAKE

 




Na mwandishi wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameungana na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa kuuaga mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Cleopa David Msuya, aliyefariki dunia siku chache zilizopita.

Ibada ya kumuaga Hayati Msuya imefanyika katika Viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliwaongoza Watanzania katika tukio hilo la kitaifa.

Akitoa salamu zake, Rais Mwinyi – kwa niaba ya Wananchi wa Zanzibar – amemuelezea Hayati Cleopa Msuya kuwa kiongozi mahiri aliyelitumikia taifa kwa uzalendo wa hali ya juu. Amesema Watanzania wamepoteza kiongozi thabiti na muumini wa dhati wa Umoja na Muungano wa Tanzania.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Hayati Msuya alikuwa kiongozi aliyeweka mbele maslahi ya Taifa, hususan katika nyakati ambapo Tanzania ilikuwa inakabiliwa na mabadiliko ya kiuchumi duniani, sambamba na juhudi za kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Rais Mwinyi ametoa wito kwa Watanzania kuyaendeleza maono ya Hayati Cleopa Msuya kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Taifa linaendelea kupiga hatua zaidi za maendeleo.

Hayati Cleopa David Msuya alifariki dunia tarehe 7 Mei 2025 akiwa na umri wa miaka 94, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, Jijini Dar es Salaam. Anatarajiwa kuzikwa katika Kijiji cha Usangi, Mwanga, mkoani Kilimanjaro, siku ya Jumanne ya wiki ijayo.








Post a Comment

0 Comments