WAZIRI KOMBO AWASILI KOSOVO KWA ZIARA RASMI

 




Na mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amewasili jijini Prishtina nchini Kosovo kwa ajili ya kuanza ziara rasmi pamoja na kushiriki Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama utakaofanyika nchini humo kuanzia tarehe 2 hadi 3 Juni, 2025.

Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Kosovo.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Prishtina, Mhe. Waziri Kombo amepokelewa na Mshauri wa Rais wa Kosovo masuala ya Sera ya Mambo ya Nje, Bi. Rejhan Vuniqi pamoja na Kaimu Mkuu wa Kituo cha Ubalozi wa Tanzania nchini Italia unaowakilisha pia nchini Kosovo, Bi. Eva Kaluwa.

Akiwa nchini humo, mbali na kushiriki mkutano huo mkubwa wa kimataifa,  Mhe. Waziri Kombo atakutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kosovo, Mhe. Dkt. Vjosa Osmani Sadriu  pamoja na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na masuala ya Diaspora wa nchi hiyo, Mhe. Donika Gervalla Schwarz.

Kadhalika Mhe. Waziri Kombo ambaye kwenye ziara hiyo amefuatana na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizarani, Balozi Swahiba Mndeme na wajumbe wengine atatembelea Chemba ya Biashara ya ushirikiano kati ya Kosovo na Marekani na kukutana na Bodi na Mwenyekiti  wa Chemba hiyo, Bw. Arian Zeka.

Aidha, wakati wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Mhe. Waziri Kombo anatarajiwa kuhutubia kwenye Jopo la Majadiliano kuhusu mada isemayo “Utangamano wa Amani katika Karne ya 21: Nini kinahitajika.

Mhe. Waziri Kombo na ujumbe wake watarejea nchini tarehe 04 Juni 2025.

Post a Comment

0 Comments